BASHUNGWA ATOA MAELEKEZO NIDA, MAOMBI VITAMBULISHO VYA TAIFA MIKOA YA PEMBEZONI.
![](http://moha.go.tz/moha9/public/images/news_images/1739442486.jpg)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na Idara ya Wakimbizi kushughulikia maombi ya Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mikoa ya pembezoni ambapo ametaka waliokidhi vigezo wazalishiwe vitambulisho na watakaothibitika hawana vigezo wapewe taarifa.
Bashungwa ametoa maagizo hayo leo tarehe 12 Februari 2025 jijini Dodoma wakati alipokutana na Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kujadili utendaji kazi na uboreshaji wa utoaji huduma wa Mamlaka hiyo.
“Muendelee kushirikiana na Idara ya Wakimbizi na Uhamiaji, kwa mikoa kama Kigoma na Kagera kushughulikia maombi yenye changamoto bila kuvunja sheria, yule ambae hajakidhi mwambieni lakini yule mwenye vigezo vya kupata kitambulisho basi apewe” amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuongeza ubunifu wa kuhakikisha vitambulisho vya Taifa vilivyozalishwa vinawafikia Wananchi husika pamoja na kuongeza kasi ya Usajili na utambuzi wa wananchi waliosalia kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi 2022.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji ameeleza kuwa NIDA inaendelea na zoezi la kusambaza vitambulisho ambavyo vilikuwa havijawafikia Wananchi ambapo kufikia tarehe 10 Februari 2025 jumla ya vitambulisho 1,507,796 vimesomeshwa kwenye mfumo na wamiliki wa vitambulisho 918,216 wameshatumiwa ujumbe mfupi ili kuchukua vitambulisho vyao.