Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI YATATHMINI MAHITAJI YA MAFUNZO KWA MAAFISA WAANDAMIZI



Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi imefanya kikao kazi cha tathmini ya mafunzo kwa Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vyake vya Usalama ambapo Lengo la kikao hicho ni kubaini changamoto wanazokutana nazo  Maafisa hao katika utekelezaji wa majukumu yao na kupokea mapendekezo namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa njia ya mafunzo, kabla na baada ya uteuzi wao katika nafasi za uongozi 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bi. Miriam Mmbaga wakati akifunga kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Dodoma kuanzia Februari 10, 2025 hadi Februari 11, 2025.

Aidha alisema kuwa tathmini hiyo itawezesha Wizara kuandaa mtaala na programu maalum ya mafunzo yatakayotolewa kwa Viongozi mara baada ya kuteuliwa na wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, kwa lengo la kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi

"Mahitaji yatakayobainishwa katika tathmini hii  yatazingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia taarifa ya Tume ya Rais ya  kuboresha haki jina,  maelekezo yaliyotolewa na Viongozi wa Kitaifa katika Semina elekezi iliyotolewa kwa Viongozi Waandamizi wa Wizara pamoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali". Amesema Bi. Miriam 

Vilevile alieleza kuwa matokeo ya tathmini hiyo yatawezesha Wizara kuandaa mfumo endelevu na mafunzo yanayolenga kuimarisha uongozi bora na uwajibikaji kwa Wizara na Vyombo vyake vya Usalama

Alihitimisha kwa kusema Mafunzo hayo kwa ajili ya Viongozi yanatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2025/2026.