BASHUNGWA AIAGIZA UHAMIJI KUENDELEA NA OPERESHENI KUWADHIBITI WAHAMIAJI HARAMU.
![](http://moha.go.tz/moha9/public/images/news_images/1737704355.jpg)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amemuagiza Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji CGI, Dkt. Anna Makakala kuendelea na Operesheni, misako na doria za kukamata wahamiaji haramu na kuhakikisha wageni wote wanaoingia ndani ya nchi, wanafuata tararibu na sheria za kuingia nchini.
Bashungwa ameelekeza hayo leo tarehe 23 Januari 2025 wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma ambapo amesema Serikali haitakuwa na muhali na mtu yeyote ambaye anaingia nchini bila kufuata Utaratibu na Sheria za Nchi yetu.
Kadhalika, Bashungwa amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji CGI, Dkt. Anna Makakala kuhakikisha kila Ofisi ya Wilaya ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inakuwa na Afisa wa Uhamiaji ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi.
“Nitakapokuwa naenda kwenye Wilaya, nikifika ofisi za NIDA nikute kuna Afisa wa NIDA lakini awepo Afisa wa Uhamiaji ambao wanashirikiana kuwahudumia Wanzania ili kuepuka usumbufu usio kuwa na tija kwa Wananchi kutoka ofisi moja kwenda ofisi nyingine” amesisitiza Bashungwa
Awali, Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji CGI, Dkt. Anna Makakala ameeleza kuwa Idara ya Uhamiaji inaendelea na misako, doria na kaguzi mbalimbali kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa.
“Katika mwaka 2024 tumefanya Operesheni, mikasako na doria nchi nzima, jumla ya Wahamiaji wa makosa mbalimbali 14,368 walikamatwa na kuchukuliwa hatua ” ameeleza CGI, Dkt. Makakala