Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

SERIKALI KUDHIBITI UHALIFU ZIWA VICTORIA



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi, amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Parvathy Sankar (Paru), Naibu Mkurugenzi Idara ya Marekani inayopambana na Madawa ya Kulevya na Utekelezaji wa Sheria (INL), akiwa ameambatana na Bi. Frances Wallman, Afisa Masuala ya Siasa wa Marekani Idara ya Afrika Mashariki na Kati, Ofisini kwake Jijini Dodoma Agosti 22, 2024.


Mazungumzo hayo yalihusiana na Mradi wa Ufadhili wa Kupambana na Kudhibiti Uhalifu katika Ziwa Victoria unaotekelezwa na Serikali ya Marekani kupitia Taasisi ya INL.


Awali kwa niaba ya Wizara Dkt. Maduhu Kazi alianza kwa kuwakaribisha na kuwashukuru kwa ujio wao huku akieleza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekuwa wakiimarisha Ulinzi na Usalama katika Ziwa Victoria kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika eneo hilo kwa Upande wa Tanzania, pia ameeleza uwepo wa Chuo cha Mafunzo ya Usalama na Uokoaji kilichopo Mwanza (Mwanza Marine College) na maeneo mengine ya maziwa makuu hivyo imechangia sana kuimarisha na kudhibiti Uhalifu kwa kutoa Mafunzo kwa Askari Polisi na Zimamoto na Uokoaji.


Aidha Naibu Katibu Mkuu alieleza baadhi ya changamoto zinazowakabili katika kupambana na Uhalifu kwenye Maziwa Makuu ambazo ni pamoja na, Uchache wa Vifaa vya Uokoaji na Doria kama vile Boti na ukosefu wa vifaa vya kujifunzia chuoni, hivyo aliomba mradi huo wa ufadhili kusaidia vifaa vya mafunzo katika chuo hicho na vifaa vingine vya ukaguzi ziwani ili kuimarisha ulinzi na usalama.


Katika hatua nyingine Dkt. Maduhu Kazi, alimuhahakishia Naibu Mkurugenzi huyo kuendelea kushirikiana na Serikali ya Marekani hususani katika kuimarisha sekta ya Ulinzi na Usalama.


Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Paru, alishukuru kupata nafasi ya kukutana na Uongozi wa Wizara kisha kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake madhubuti za kupambana na Uhalifu kwenye Maziwa Makuu.


Ndg. Naibu Katibu Mkuu natambua huu ndio mwaka wa mwisho wa mradi huu, ninayo furaha kueleza kuwa Serikali ya Marekani kupitia Idara ya INL ipo tayari kuendelea kufadhili mradi huu muhimu kwa kipindi kingine cha miaka mitatu baada ya kufanya tathimini ya mradi sambamba na kukusanya maoni kutoka kwa wadau wa mradi huo ambao unahusisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.


Bi. Paru alisisitiza kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya Uhifadhi, Ulinzi na Usalama wa Ziwa Victoria na ameahidi kuwasilisha maombi ya Serikali kupitia Wizara husika, kwa Taasisi za INL na IOM ili kuchochea Usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu na kutembelea Maziwa mengine ya Nyasa na Tanganyika ili yaweze kunufaika na mradi huo.