Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KATORO KUPATIWA WILAYA YA KIPOLISI NA KUJENGEWA KITUO CHA POLISI



KATORO KUPATIWA WILAYA YA KIPOLISI NA KUJENGEWA KITUO CHA POLISI 

Na Mwandishi wetu;- 

Serikali imesema itaupatia Mji mdogo wa Katoro Mkoa wa Geita Wilaya ya Kipolisi na kuujengea Kituo kipya cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya ili kuimarisha Ulinzi na Usalama wa raia na mali zao.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa Mkoani Geita.

Naibu Waziri Sillo, amesema sababu za kupeleka hitajio hilo ni kutokana na Mji wa Katoro wenye watu zaidi ya laki tatu kukua kibiashara na kiuchumi kwa kasi.

"Kituo cha Polisi kilichopo kipo katikati ya makazi ya watu na maeneo ya biashara habari njema ni kwamba IGP alituma timu yake hapa walishafanya tathimini hivyo mnajengewa Kituo kipya cha kisasa na mnapatiwa Wilaya ya Kipolisi hapa Katoro"Alisema

Aidha, Sillo amewahimiza Polisi kata nchini kuendelea kutoa elimu ya Polisi jamii kwa Wananchi na Viongozi wa Serikali za mitaa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ili kupambana na kutokomeza uharifu unaojitokeza maeneo mbalimbali ikiwemo wizi wa mifugo unaotajwa kuwepo kwa wingi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

"Wananchi mnapata taarifa za wezi, mnakaa nazo na wengine kuishi nao naomba toeni taarifa kwa Jeshi la Polisi ili sheria ichukue mkondo wake"Alisema Mhe. Sillo.