Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

GUGU:WAALIMU SIMAMIENI MAADILI BORA YA WANAFUNZI HILI NI TAIFA LA KESHO



GUGU:WAALIMU SIMAMIENI  MAADILI BORA YA WANAFUNZI HILI NI TAIFA LA KESHO

Na Mwandishi Wetu;-

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu ameiasa Jamii kurudi katika misingi ya Utanzania na kuhakikisha kuwa suala la Mmomonyoko wa Maadili linapewa kipaumbele kuanzia ngazi ya familia ili kizazi cha sasa na cha baadaye kiendelee kubaki salama na kujenga Taifa lenye watu waliostaarabika


Gugu ambaye alikua Mgeni Rasmi ametoa nasaa hizo katika Mahafali ya darasa la Saba ya Shule ya Martin Luther yaliyofanyika Agosti 10, 2024 Jijini Dodoma


Gugu amesisitiza kuwa kwa sasa nchi inakabiliwa na janga la Mmomonyoko wa Maadili ambalo kwa kiasi kikubwa linaathiri jamii.

“Nitumie fursa hii kuiasa Jamii kwa ujumla kurudi katika Misingi yetu ya Kitanzania na kuhakikisha kuwa suala hili la Mmomonyoko wa Maadili tunalipa kipaumbele ili watoto wetu waendelee kubaki salama na hatimaye kujenga Taifa lenye watu wastaarabu” Alisema Gugu.


Aidha, ameitaka Shule hiyo kuzingatia misingi muhimu iliyowekwa na Serikali katika kuwaandaa watoto ikiwa ni pamoja na kuwajenga wanafunzi wenye uwezo wa kuwasiliana kwa lugha fasaha kama lugha ya Taifa (Kiswahili) lugha za Kigeni ikiwemo Kiingereza, Lugha ya Alama, Breli na lugha ya Mguso.


Awali Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Gilbert  Nhuguti Alisema Jumla ya wanafunzi 195 wakiwemo wasichana 102 na wavulana 93 ndio wanaotarajiwa kuhitimu masomo yao ya Darasa la Saba Shuleni hapo ambapo kwa wakati wote Shule imechukua jukumu la kuwajenga kimasomo na Kimaadili. 


Ameongeza kuwa Lengo Kuu la Shule hiyo ni kutoa elimu bora inayojenga misingi imara na endelevu kwa watoto katika makuzi ya kiroho, Kimwili na kiakili ili kuwaandaa vijana kuwa Raia wema wenye Uadilifu, Uzalendo na hofu ya Mungu


“Shule hii inalenga kuwaandaa watoto katika misingi imara ya kiroho, kimwili na kiakili” Alisema.


Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imefanya maboresho katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 kwa lengo la kuwa na mfumo wa Elimu na Mafunzo unaoweza kumuandaa Mtanzania Mwenye Maarifa, Stadi na mtazamo chanya utakaomuwezesha kuchangia kuleta maendeleo endelevu kwa Taifa


Miongoni mwa maboresho hayo, ni pamoja na kukuza maarifa, ujuzi na mwelekeo wa kutunza mazingira, kuheshimu usawa wa kijinsia na kumuezesha mwanafunzi kutambua masuala mtambuka.