Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

KATUBU MKUU, GUGU ALITAKA JESHI LA POLISI KUSIMAMIA MIRADI YA SERIKALI KWA WELEDI



Katibu Mkuu, Gugu alitaka Jeshi la Polisi kusimamia Miradi ya Serikali kwa Weledi

Na Mwandishi Wetu;-

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu amewataka Maofisa, Wakaguzi na Askari wa Vyeo mbalimbali Jeshi la Polisi  kutumia vizuri fedha za miradi wanazopewa na Serikali kwa weledi na viwango ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati kwa sababu hiyo ndio njia pekee ya kuweza kutoa shukrani kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo 


Gugu amezungumza hayo katika kikao kazi alipofanya ziara yake ya kwanza tangu uteuzi wake katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kupokelewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura na baadaye kutembelea mradi wa nyumba za makazi ya askari Polisi unaendelea kujengwa jijini Dodoma Julai 31, 2024 


Katibu Mkuu amesema kuwa tunapoanza utekelezaji wa bajeti katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 Jeshi la Polisi linatakiwa kuongeza viwango zaidi katika miradi yao pia aliwahimiza kufanya maombi ya fedha za miradi hiyo kwa wakati ili iwezekukamilika kwa muda uliokusudiwa.


Aidha, Gugu alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea  kutambua majukumu yao ya kulinda usalama wa Raia pamoja na mali zao ipasavyo


"Sisi kama Wizara tunatambua kazi kubwa na adhimu ambayo mnaifanya na tutaendelea kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya hongereni sana." Amesema


Gugu amewataka Watumishi wa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa wazalendo na kuifanya kazi yao kizalendo kwa sababu nchi inapokuwa na amani na utulivu shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii zitaendelea vizuri hasa pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anapohamasisha utalii, hao watalii hawataweza kufanya shughuli zao za kiutalii ikiwa hakuna kwa amani na utulivu


Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi, IJP Camilius Wambura alianza kwa kutoa taarifa ya hali ya usalama nchini ambapo alisema nchi ipo salama licha ya hivi karibuni kuibuka malalamiko ya watoto kufanyiwa vitendo vya kikatili pamoja na unyanyasaji dhidi ya kina mama lakini vyote vimeshughulikiwa


Alihitimisha kwa kusema Jeshi la Polisi limejiwekea utaratibu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi na nidhamu ili wananchi wapate haki na matokeo mazuri ya kazi ya Jeshi la Polisi.