Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

SERIKALI KUFANYA TATHIMINI YA UREJEAJI WA HIARI WA WAKIMBIZI IFIKAPO JANUARI, 2025




SERIKALI KUFANYA TATHIMINI YA UREJEAJI WA HIARI WA WAKIMBIZI IFIKAPO JANUARI, 2025 

Na Mwandishi Wetu;

Serikali imesema katika kuhakikisha kuwa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini wanapata suluhisho la kudumu ifikapo Januari 2025 itafanya zoezi la mahojiano ili kutoa fursa ya kuwasikiliza Wakimbizi hao na kufanya maamuzi sahihi kuhusu hadhi zao kwa kuzingatia sheria za ndani, kikanda na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 7, 2024 Mkoani Kigoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, wakati akihitimisha ziara yake na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Mhe. Nibona Bonansize katika kambi za wakimbizi za Nyarugusu na Nduta Mkoani humo.

Mhe. Sillo alisema Serikali itachukua hatua hiyo endapo Idadi ya Wakimbizi wanaojitokeza kurudi kwao kwa hiari itaendelea kuwa ndogo baada ya mawaziri hao kufanya Mikutano miwili na wakimbizi na kuelezwa hali ya usalama katika nchi yao ya Burundi. 

“Urejeaji huu ni wa hiari kama yalivyo makubaliano yetu lakini kama Serikali tunatoa wito na tunasisitiza warudi wakaijenge nchi yao ya Burundi kwani kwa sasa iko salama”Alisisitiza Mhe. Sillo.

Aidha alisema Serikali ina mpango mahsusi baada ya muda huo kwenda nyumba kwa nyumba kufanya tathimini ya kila mkimbizi kujua tatizo ni nini, kwanini amekimbia na kwanini anakuwa na mashaka ya kurudi nchini kwao na wakati nchi iko salama.

“Tutafanya tathimini ya kutosha mtu kwa mtu, familia kwa familia na kuhakikisha tunapata sababu za kutosha kwamba kwanini hawataki kurudi nyumbani lakini tunaendelea kuhamasisha kwamba lengo na nia ni kuhakikisha wanarudi salama nyumbani kwao kwenye nchi yao ya asili ya Burundi” Alisema Mhe. Sillo.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia wa Burundi, Mhe. Nibona Bonansize, alisema hali ya kiusalama nchini humo ni salama na shughuli za kimaendeleo zinaendelea vyema hivyo kuwataka kurejea nyumbani kusaidia kulijenga Taifa lao kiuchumi.

“Ifikapo mwaka 2060 tunatarajia kuwa mbali zaidi hivyo hatuna sababu ya Warundi kuendelea kuwa nje ya nchi bali warejee nchini ikiwa ni pamoja na idadi hii kubwa ya Watoto na Vijana ambao ni tegemeo na nguvu kazi ya Taifa”Alisema Mhe. Bonansize.

Vilevile aliwataka wazazi kuamua kurejea nyumbani ili kuhakikisha watoto wanapata elimu na haki zao za msingi kwani kuendelea kubaki kambini wanazidi kukosa haki zao za kimsingi ikiwa ni pamoja na kupata elimu bora.

Itakumbukwa kuwa kwenye Mkutano wa 24 uliohusisha pande tatu Serikali ya Tanzania, Burundi na UNHCR, uliyofanyika Novemba, 2023 Jijini Dar es Salaam na kuazimiwa kuwa wakimbizi 2,000 wawe wanarejea kwa wiki lengo ambalo halijawahi kufikiwa.