RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 62 YA UHURU
Tarehe 09 Disemba, 2023 Taifa letu linaadhimisha
Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Hili ni tukio la muhimu na la
kihistoria kwa Taifa letu. Katika kuadhimisha sherehe hiyo, Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametumia
Mamlaka aliyopewa chini ya Ibara 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti yafuatayo:-
1. (i) Wafungwa
wote wenye sifa
stahiki wamepunguziwa robo (1/4) ya
adhabu baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya kifungu cha
49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. Wafungwa hao ni wale waliohukumiwa kifungo cha kuanzia miaka
miwili na kuendelea na ambao wametumikia robo (1/4) ya
adhabu zao gerezani na ambao waliingia gerezani
kabla ya tarehe
12 Oktoba, 2023 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika sharti la 2(i
– ix);
(ii)
Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa
ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho (Terminal Stage). Ugonjwa
na hatua hiyo vimethibitishwa na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;
(iii)
Wafungwa wa maisha ambao
wametumikia vifungo vyao kwa muda wa miaka kumi na tano (15) na kuendelea.
Aidha, kwa wafungwa wote waliobadilishiwa adhabu (commuted) hesabu zao
zihesabike kuanzia tarehe ya kubadilishiwa adhabu;
(iv)
Wafungwa wa kunyongwa waliomaliza
taratibu za Kimahakama na ambao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka kumi (10) na
kuendelea kusubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo waliobadilishiwa
kifungo kutoka cha kunyongwa kwenda kifungo cha maisha;
(v)
Wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua, kujaribu
kujiua au kuua watoto wachanga (Attempt
to Murder, Attempt Suicide or Infanticide) ambao wametumikia nusu
ya adhabu zao na kwa waliohukumiwa kifungo cha
maisha masharti ya aya ya 1(iii) hapo juu
yametumika;
(vi)
Wafungwa wazee wenye umri wa miaka
sabini (70) au zaidi ambao wametumikia robo (1/4) ya
adhabu zao, baada ya umri wao kuthibitishwa
na jopo la waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga
Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;
(vii)
Wafungwa wa kike walioingia na
mimba gerezani au wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya;
(viii)
Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na
akili wasio na uwezo
wa kufanya kazi, baada ya ulemavu wao kuthibitishwa na
jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga
Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya;
(ix)
Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya
kuwekwa kizuizini (Under Presidential Pleasure) ambao wamekaa gerezani kuanzia
miaka kumi (10) au zaidi;
2. Aidha,
msamaha huo haukuwahusisha wafungwa wafuatao:-
(iii)
Wafungwa wanaotumikia vifungo vya
nje chini ya Sheria ya Bodi za
Paroli Sura ya 400 (R.E 2002), Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E,
2002) na Kanuni za kifungo cha nje {The Prisons (Extra Mural Penal Employment)
Regulations, 1968};
(iv)
Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo kwa mashauri/kesi za uhujumu uchumi na wale wanaotumikia vifungo kwa makosa ya matumizi
mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa, usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na madawa ya
kulevya ikiwemo bangi;
(v)
Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka,
kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yale yanayohusiana na ukatili
dhidi ya
watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile na biashara haramu ya
binadamu;
(vi)
Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa vifungo kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi,
unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi
wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu
kutenda makosa hayo;
(vii)
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa
makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili;
(viii)
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa
makosa ya wizi/ubadhilifu wa fedha za Serikali;
(ix)
Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa
makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka
chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo;
(x)
Wafungwa warudiaji;
(xi)
Wafungwa waliowahi kupata msamaha
wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania isipokuwa kwa wafungwa walioainishwa katika sharti la 1(iii),(iv) na
(xii)
Wafungwa wa
Madeni (Civil Prisoners).
Wafungwa 2,244 wamenufaika na Msamaha huu ambapo
wafungwa 263 wataachiliwa huru leo tarehe
09/12/2023, wafungwa 2 waliohukumiwa
adhabu ya kifo wamebadilishiwa adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha na
wafungwa 1,979 wamepunguziwa sehemu
ya adhabu zao ambazo wataendelea kuzitumikia gerezani. Ni matumaini ya Serikali kwamba wafungwa
walioachiliwa huru leo tarehe 09/12/2023 watarejea tena katika jamii
kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na kwamba
watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.