SAGINI AAGIZA POLISI MARA KUTOA GARI KWA AJILI YA KUBEBA MAHABUSU GEREZA LA BUNDA
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mb), Jumanne Sagini ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kutoa gari la kusafirisha mahabusu waliopo katika Gereza la Wilaya Bunda na kuwapeleka kwenda Mahakama ya Wilaya Butiama ikiwa ni pamoja na kuwarudisha ili wapate haki yao.
Sagini alitoa maagizo hayo Novemba 19, 2023 wakati alipotembelea Gereza la Bunda na kuongea na wafungwa pamoja na mahabusu wa Gereza hilo ambapo alikutana na changamoto ya mahabusu waliokwama kwenda Mahakamani kwa kukosa usafiri.
"Kuwa hapa Gerezani haimanishi ukose haki yako na haki yako utaipata Mahakamani kwani kuna watu wamo humu lakini ilipaswa wawe uraiani."
"Wapo waliofungwa pakubwa ilipaswa iwe kidogo na wengine wamefungwa padogo ilipaswa wafungwe pakubwa hivyo gari la Polisi litoke Mkoani na kuwapeleka Mahakamani," alisema Sagini
Naibu Waziri Sagini yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ambapo anatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Ujenzi inayoendalea ndani ya vyombo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inayolenga kutatua changamoto mbalimbali za Wananchi.