BARAZA DOGO LA WAFANYAKAZI WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI LAKUTANA KUPITIA MPANGO WA BAJETI KWA MWAKA 2023/24 NA TAARIFA YA UTEKELEZAJI KUANZIA JULAI 2022-JANUARI 2023.
Baraza dogo la
Wafanyakazi Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi limekutana na kupitia mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 pamoja na
taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kuanzia Julai 2022 –Januari 2023 kwa
mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha
mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu Miriam P. Mbaga ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema kuwa
matarajio ya Baraza hilo ni kuhakikisha kuwa Watumishi wanashiriki na kutoa
maoni, ushauri na mapendekezo yao ipasavyo ili kuboresha mazingira ya utendaji
kazi na kuboresha maslahi ya Watumishi na kufanikisha ufanisi na utendaji bora
wa Wizara kwa Wananchi.
Akifungua Baraza hilo Katibu Tawala
Mkoa wa Dodoma Dk Fatuma Mganga ameliomba Baraza hilo kuhakikisha kuwa
wanasimamia na kuhamasisha utekelezaji wa majukumu kuzingatia kiapo cha ahadi ya uadilifu na kuweza kutumia
rasilimali zilizopo katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu.
“Rai yangu kwenu tutumie mikutano ya Baraza la Wafanyakazi
kujadili mambo yatakayoimarisha utendaji kazi ili kufikia malengo ya Wizara na
Serikali kwa ujumla. Tujue kwamba tunawatumikia Watanzania wenzetu. Panapoibuka
changamoto na malalamiko ndani ya Wizara tujue kwamba kuna mmoja wetu ambaye
hajatekeleza majukumu yake vizuri. Ni kazi ya Baraza kukumbushana ili utendaji
wetu wa kazi uwe na tija.” alisema Dk Mganga.
Aliendelea kusema kuwa, “Kama tunavyofahamu bajeti ni nyenzo muhimu
katika utekelezaji wa mipango ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu na pia
kufikia katika muda uliopangwa na kutoa matokeo tarajiwa. Wakati wote rasilimali
huwa haitoshi lakini inapaswa kutumia rasilimali zilizopo kufanya utekelezaji
wa majukumu kulingana na vipaumbele.”
Katika hatua nyingine Mganga amehimiza uwepo wa mahusiano mema kati
ya Watumishi kwa Watumishi na Watumishi
na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali kwani mahusiano ndio mtaji katika
kufanikisha utendaji kazi. Aidha, amewasisitiza Viongozi kuacha ubinafsi na
kusimamia maslahi ya wanaowaongoza kwa kuhakikisha kuwa kila Mtumishi anapata anachostahili ili kuwa na
mahusiano bora katika eneo la kazi.
Wakizungumza na kutoa tathmini ya
mkutano wa Baraza hilo la Wafanyakazi baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi akiwemo Francis Rubert ambaye pia ni Katibu wa Baraza dogo la Wafanyakazi Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi amesema kuwa mkutano huo umekuwa ni wa manufaa makubwa
kwao kwani kupitia mkutano wa baraza hilo mambo mengi yameweza kuelekezwa kwa
ajili ya kuboresha ufanisi katika utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kukumbushwa
wajibu wa utendaji kazi kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
Boaz Mwazyunga Katibu wa TUGHE tawi
la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi amesema kuwa Baraza limekuwa likisaidia utekelezaji
wa masuala mbalimbali ya Kiutumishi ndani ya Wizara na masuala hayo yamekuwa yakizingatiwa kwa uwazi na kumekuwa
na mgawanyo wa matumizi kwa
kuwashirikisha Watumishi na kuhimiza usawa miongoni mwa Watumishi wa Wizara.
Ikumbukwe kuwa mkutano huo wa Baraza
unalengo la kupitia mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 pamoja na taarifa ya
utekelezaji wa mpango na bajeti kuanzia Julai 2022 –Januari 2023 kwa mwaka wa
fedha 2022/2023.