Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MASAUNI ATAKA ASKARI POLISI WAPYA KUFANYA KAZI KWA WELEDI, AWAMU YA SITA KWA MIAKA MITATU YAAJIRI 15,946



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameviwezesha vyombo vya ulinzi katika kuongeza idadi ya askari ambao wanakwenda kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania.

Hayo ameyasema leo Machi 25, 2024 Moshi katika Shule ya Polisi Tanzania na Waziri Masauni wakati akifunga mafunzo ya awali ya askari Polisi katika kambi ya Kilelepori Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Mhandishi Masauni amewataka askari kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi huku akiwataka kuwa mfano kwa askari watakao wakuta katika Mikoa na vituo vya kazi watapopangiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi wanakokwenda.

Pia Waziri Masauni amesema katika miaka mitatu ya Rais Samia, ameajiri askari 15,946.

 "Katika miaka mitatu pekee ya Serikali ya Awamu ya Sita imeajiri jumla ya askari wapya 15,946 na watumishi raia 80 kwa ajili ya Wizara na Vyombo vyake vya Usalama, ambapo kati ya hao 11,226 sawa na asilimia 70 wameajiriwa katika Jeshi la Polisi," alisema Masauni.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Fedha na Logistiki CP Liberatus Sabas ambaye amemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini amewataka askari hao wapya kutambua kuwa askari ni kioo cha  Jamii ambapo amewataka kwenda kutatua changamoto za wananchi wanaolitegemea Jeshi hilo.

Kamishna wa Polisi Operesheni mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji amebainisha kuwa mafunzo ya kijeshi yanahitaji uvumilivu na nidhamu kubwa ili uweze kufaulu mafunzo hayo ambapo amesema wataendelea kuwafundisha askari hao wakiwa kazini ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji.

Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Ramadhan Mungi amesema askari hao wamefundishwa mambo mengi ambayo yamewajenga kitaluma na kijeshi huku akibainisha kuwa wapo wanafunzi ambao wamefukuzwa mafunzo kwa kutokizi viwango vya Jeshi hilo ambao Jumla yao ni 193.