AYOUB ATOA MIKAKATI MIPYA KUIMARISHA USALAMA BARABARANI
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema Serikali inaendelea kuimarisha usalama barabarani nchini kupitia usimamizi madhubuti wa leseni za udereva, hususan kwa madereva wa mabasi na malori wenye leseni za Madaraja C na E.
Akizungumza jijini Dodoma leo, katika kikao cha kwanza cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Ayoub amesema madereva wa vyombo hivyo wana jukumu kubwa katika kulinda maisha ya wananchi na mali zao kutokana na kubeba abiria wengi pamoja na mizigo mikubwa, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zote za usalama barabarani ikiwemo uhuishaji wa leseni kwa wakati.
Aidha, amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji ili kusikiliza changamoto zilizopo na kuboresha mifumo ya usalama barabarani kwa lengo la kuongeza ufanisi, na usalama kwa watumiaji wote wa barabara nchini.
Naye, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, SACP William Mkonda amesema Mfumo wa Ukaguzi wa Vyombo vya Moto na Utoaji wa Stika za Kielektroniki (MIVIS) umeongeza ufanisi mkubwa katika ukaguzi wa vyombo vya moto na usimamizi wa taarifa za magari nchini.
Ameongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yamerahisisha utoaji wa huduma na kuongeza uwezo wa udhibiti wa vyombo vya moto, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa sheria za usalama barabarani kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa.
