AYOUB: UBUNIFU NA UBORA WA BIDHAA NI UFUNGUO WA USHINDANI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema ubunifu, ubora wa bidhaa na kuzingatia viwango vya kimataifa ni nguzo muhimu zitakazowawezesha wafanyabiashara na wazalishaji kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Siku ya Zanzibar kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Saba Saba), Mhe. Ayoub amesema Maonesho ya hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji na uzalishaji kwa kuwakutanisha wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali.
Amesema ushiriki wa Zanzibar katika maonesho hayo umechangia kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa visiwani, kuonesha ubunifu wa Wazanzibari na kufungua fursa za ushirikiano wa kibiashara na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Mhe. Ayoub amesema Serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji kuboresha ubora wa bidhaa, vifungashio na uzalishaji ili kunufaika na masoko ya Afrika Mashariki, pamoja na masoko mengine ya kimataifa.
