Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

SERIKALI YAKABIDHI MAGARI 13 KWA IDARA YA UHAMIAJI



Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imekabidhi magari 13 kwa Idara ya Uhamiaji kwa lengo la kuboresha huduma za kiusalama na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Januari 13, 2025 Ofisi za Idara ya Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Daniel Sillo amepongeza juhudi za Idara ya Uhamiaji katika kutenga bajeti kila mwaka kwa ununuzi wa vyombo vya usafiri aliongeza kuwa hatua hiyo inaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Pongezi hizi zinatokana na misingi mizuri iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo kila mwaka imeendelea kuongeza bajeti katika vyombo vya usalama ili kuviwezesha kutekeleza majukumu yake ya msingi. Hatua hizi ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, kupitia Ibara ya 105 inayoelekeza kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uwezo wa Vyombo vya Usalama,” Amesema Sillo

Naibu Waziri alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara ya Mambo ya Ndani imetenga jumla ya Shilingi bilioni 46.2 kwa ajili ya ununuzi wa magari mapya 435 yatakayosaidia Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara hiyo, ikiwemo Idara ya Uhamiaji ambayo imetengewa Shilingi bilioni 3.2 kwa ununuzi wa magari 11.

Aidha, alisisitiza kuwa magari hayo yatasaidia kuongeza ufanisi wa kazi za kiusalama na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku akitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha magari hayo yanatunzwa vizuri na kutumika kwa shughuli zilizokusudiwa

Naye, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msaada wagari hayo ambapo amesema magari hayo yatakuwa chachu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya Idara hiyo hasa katika suala la kufanya doria na misako ya mara kwa mara katika maeneo yote ya nchi yetu

Awali Kamishna wa Fedha na Utawala wa Idara hiyo Hamza Shaban alieleza kuwa Magari hayo ni moja ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya awamu ya Sita ya Mwaka 2021/2022 hadi leo ambapo alimshukuru Rais kwa kuitengea Idara hiyo kiasi cha Bilioni 13 ambayo itasaidia Idara hiyo kupata jumla ya magari 60.