MAKALA: LEO NI MAADHIMISHO YA SIKU YA WAKIMBIZI DUNIANI

Tuesday, June 20, 2017

LEO NI MAADHIMISHO YA SIKU YA WAKIMBIZI DUNIANI
 
Na Christina Mwangosi, MOHA
Tarehe 20 mwezi Juni ya kila mwaka hufanyika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambapo Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kila mwaka huku Maadhimisho hayo yakilenga kuhamasisha mataifa mbalimbali kuendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi wanaokimbia nchi zao za asili kutokana na machafuko na majanga mbalimbali kama ambavyo Mikataba ya Kimataifa inavyoendelea kusisitiza juu ya kuendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi .
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambalo kwa hapa nchini hufanya kazi za Kuwahudumia Wakimbizi kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Huduma za Wakimbizi  kwa mwaka huu Maadhimisho hayo yatafanyika jijini Dar es salaam huku kauli mbiu ya mwaka huu wa 2017 ikiwa ni ‘Tupo Pamoja Na Wakimbizi’  ‘We Stand Together With Refugees’
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi ambao wamelazimika kuyahama makazi yao  kwa sababu ya vita na machafuko na kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kiasi cha watu 43 milioni duniani kote wamelazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya vita, machafuko au majanga ya asili, na kati yao kiasi cha milioni 10 wanahudumiwa na Shirika hilo.
Katika kipindi cha mwaka 2016/17 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini na wadau wengine, imeendelea kutoa hifadhi na huduma kwa wakimbizi kutoka nchi jirani, hususan zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la wakimbizi hao.
 
Aidha, hadi kufikia tarehe 5 Juni, 2017 idadi ya wakimbizi wanaohifadhiwa hapa nchini  imefikia wakimbizi 344,542 ambao wamehifadhiwa katika kambi za Nyarugusu, Nduta, Mtendeli zilizoko katika Mkoa wa Kigoma na wengine katika makazi ya Katumba, Mishamo, Ulyankulu na Chogo  ambapo hawa ni wale waliokosa fursa ya kupata uraia wa Tanzania.
 
Mkurugenzi wa Idara ya Kuhudumia Wakimbizi nchini Idara ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Harrison Mseke, anasema kuwa Serikali inaendelea kupokea Wakimbizi wapya kutoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwamba awali, wakimbizi kutoka Burundi walikuwa wakipokelewa moja kwa moja kwenye kambi bila ya kufanyiwa mahojiano ya kina kutokana na kuingia kwa makundi makubwa kwa sababu ya machafuko ya kisiasa yaliyokuwa yanaendelea nchini kwao.
 
Hata hivyo Mkurugenzi Mseke anasema  baada ya kubainika kuwa hali ya usalama nchini Burundi imeimarika kwa sasa na wengi wa wakimbizi hawa wanakimbilia Tanzania kwa sababu za kiuchumi, hususan kutokana na ukame ulioikumba sehemu kubwa ya nchi hiyo na kusababisha njaa, mapema mwezi Februari, 2017 Serikali ya Tanzania ilisitisha utaratibu wa kuwapokea na kuwasajili wakimbizi bila ya kuwahoji kwa kina (prima facie recognition) na kuendelea na utaratibu wa kawaida wa kila mkimbizi kuhojiwa na Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kujadili Maombi ya Waomba Hifadhi (National Eligibility Committee) na kwamba lengo la utaratibu huu wa kumhoji kila muomba hifadhi ya ukimbizi ni kuhakikisha kuwa Serikali inatoa hifadhi ya ukimbizi kwa wanaostahili tu.
 
Pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania kuendelea kuhifadhi na kuwahudumia wakimbizi ili kutekeleza ahadi ama Mikataba mbalimbali ya Umoja wa Mataifa ambazo Serikali ilitia saini ‘‘Serikali kwa kushirikiana na UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) inaendelea kutekeleza mradi wa kuwahamishia nchini Marekani wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wanaishi katika kambi ya Nyarungusu, ambapo kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2017 wakimbizi 6,983 walikuwa wamehamishiwa nchini humo’’. Anasisitiza Mkurugenzi Mseke. 
 
Anasisitiza kuwa pamoja na mpango wa kuwapeleka wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Marekani, jumla ya wakimbizi 227 walihamishiwa katika nchi za Australia (23), Canada (427), Uingereza wawili (2) na Sweden watano (5) huku lengo la kuwahamishia wakimbizi hao katika nchi hizo likiwa ni kuzipunguzia mzigo nchi zenye wakimbizi wengi ikiwemo Tanzania.
 
Pamoja na changamoto mbalimbali katika kuwahudumia na kuwahifadhi wakimbizi mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2012 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilifanikiwa kuifunga Kambi ya Mtabila  na kubaki Kambi moja tu ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma  iliyokuwa na wakimbizi zaidi ya 35,000 kutoka nchi ya Burundi. Kwa sasa Tanzania imebakiwa na Kambi tatu za Wakimbizi ikiwemo ya  Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma ambayo ina zaidi ya Wakimbizi 65,084 wengi wao wakiwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Nduta pamoja na Mtendeli zilizopo Mkoa wa Kigoma. Hata hivyo mapema mwezi Aprili, mwaka 2015 wimbi la Wakimbizi  wapya kutoka nchini Burundi liliingia tena nchini Tanzania hivyo hadi kufikia Juni 5, 2017  idadi ya Wakimbizi imefikia 344,542.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira anasema kuwa,  kwa kuwa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo nchini Burundi imeimarika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imependekeza kuwepo kwa mazungumzo kati yake na Serikali ya Burundi pamoja na UNHCR, lengo likiwa ni kuwawezesha wakimbizi watakaopenda kurejea kwao kwa hiari na kusaidiwa kujenga maisha mapya katika nchi yao ya asili kurejea katika nchi zao za asili.
 
Meja Jenerali Rwegasira anaongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2016/17 UNHCR   kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza zoezi la kuwasajili wakimbizi wanaoishi nchini ambapo katika hatua ya awali zoezi hilo litahusisha kuwapatia namba za utambuzi ili kubana mianya ya wakimbizi kudanganya na kusajiliwa kama raia nchini Tanzania.
 
Meja Jenerali Rwegasira anasema NIDA imepanga kutekeleza zoezi hilo kabla ya kuanza usajili wa raia wa Tanzania katika Mkoa wa Kigoma ambako kuna kambi nyingi za wakimbizi huku lengo likiwa kuwapatia wakimbizi hao Vitambulisho vya Taifa vitakavyowawezesha kupata huduma mbalimbali wanazostahili.
 
‘‘Kuwapatia wakimbizi hati za utambulisho pamoja na kusaidia utambulisho ni kutekeleza mikataba ya kimataifa ambapo wakimbizi wanapaswa wawe na hati muhimu kama hitajio muhimu kulingana na Mikataba ya Kimataifa’’. Anasisitiza Meja Jenerali Rwegasira.
 
Meja Jenerali Rwegasira anasema kuwa, Serikali ilitoa uraia kwa wakimbizi 162,156 wenye asili ya Burundi walioingia nchini mwaka 1972 na kupangiwa kuishi katika makazi ya Katumba, Mishamo mkoani Katavi na Ulyankulu mkoani Tabora na kwamba kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa utangamanisho (local integration), ambao utawahamasisha raia hao kuhamia katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
 
Kutokana na hali hiyo, ‘‘Serikali inaendelea kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kutimiza wajibu wake katika kutekeleza mradi wa utangamanisho kwa kuchangia rasilimali zinazohitajika kuwezesha raia hao kuwa sehemu ya jamii watakayohamishiwa’’. Anasisitiza Meja Jenerali Rwegasira.
 
Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba, anasema kuwa ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata  nishati ya kupikia, fito  za kujengea  katika maeneo ya ndani ya kambi  na maeneo yanayozunguka kambi hizo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na UNHCR imeanza kutekeleza mradi wa kutumia majiko ya gesi kupikia badala ya kuni katika kambi ya Nyarugusu kwa awamu ya kwanza, ambapo mitungi ya gesi 3,216 imegawiwa kwa wakimbizi.
 
Hatua hii ilitokana na Serikali ya Tanzania katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 kuahidi kutekeleza miradi inayolenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia, fito za kujengea na kuhamasisha upandaji wa miti katika maeneo ya ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo.
 
Waziri Mwigulu anasema  katika kupunguza na kukabiliana na uharibifu wa mazingira  jumla ya miche ya miti 1,481,592 imekuzwa na kupandwa ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo.
 
Anaongeza kuwa kwa sasa ujenzi wa nyumba 15,664 ambazo zitatumia tofali mbichi na kuezekwa kwa kutumia mabati badala ya kutumia fito za miti ambazo zinachangia katika uharibifu wa mazingira unaendelea katika kambi hizo.
 
‘‘Wizara yangu kupitia Idara yake ya Kuhudumia Wakimbizi itaanza kutekeleza mradi wa matumizi mbadala ya mkaa katika kambi za wakimbizi, kufuatia kukamilika kwa utafiti wa upatikanaji wa malighafi za uzalishaji ambapo jumla ya majiko sanifu 59,924 yamegawiwa kwa kila nyumba katika kambi za Wakimbizi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli...hii tunalenga kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya kambi za wakimbizi hapa nchini’’. Anasisitiza Mwigulu.
 
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi na Jumuiya ya Kimataifa linaamini suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi ni kwa wakimbizi kupata nafasi ya kurejea kwao kwa hiari, mara baada ya mazingira yaliyowafanya kuzikimbia nchi zao  za asili kutoweka.  Jambo hili litafanyika na kufanikiwa pale Serikali za nchi na Jumuiya ya Kimataifa zitakapochukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa sababu zinazowafanya raia wa nchi mbalimbali kuzikimbia nchi zao zinatafutiwa ufumbuzi.  Hii ni pamoja na kuwa na Serikali zinazozingatia sheria, utawala bora na haki za binadamu.
Aidha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kupokea wakimbizi mapema kabla ya kupata Uhuru wake na kwamba ni miongo mitano sasa imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka katika Nchi za Maziwa Makuu hali iliyosababisha kufunguliwa kwa kambi na makazi ya wakimbizi 17 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
 
Kati ya kipindi cha miaka ya 1960 na 1980,  nchi ya Tanzania  ilipokea wakimbizi kutoka nchi jirani za Burundi na Rwanda pamoja na wale Wakimbizi wapigania uhuru kutoka nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, wakimbizi hawa walihifadhiwa katika makazi na vijiji vya watanzania. Hata hivyo kati ya miaka ya 1990 nchi ya Tanzania pia ilipokea makundi makubwa ya wakimbizi kutoka nchi jirani za Burundi, Rwanda na DRC ambapo wakimbizi hawa tofauti na wale wa miaka ya nyuma walihifadhiwa katika kambi za wakimbizi kutokana na sababu za kiusalama.
 
Hata hivyo baada ya nchi nyingi kupata Uhuru ikiwemo pia hali ya Amani kurejea katika nchi za Burundi na Rwanda, wakimbizi wengi walirejea katika nchi zao za asili hali iliyowezesha nchi ya Tanzania kuzifunga kambi zipatazo 11 za wakimbizi na kubakiwa na kambi moja tu ya Nyarugu ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka jamhuri ya kidemokrasia ya kongo-DRC.
 
Aidha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikihifadhi na kuwahudumia wakimbizi kwa kutumia mifumo miwili tofauti ukiwemo ule wa kuwahifadhi katika kambi za wakimbizi ambapo wakimbizi hupewa misaada ya kibinadamu na kuhudumiwa kila kitu na miundombinu yake huwa ni ya muda mfupi kwa kutarajia kuwa amani itakaporejea kwenye nchi zao za asili wakimbizi hao kwa hiari yao watarejea kwenye nchi zao huku  mfumo wa pili ni ule wa makazi ambapo  wakimbizi huruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi na miundombinu yake huwa ni ya kudumu.
 
Pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kushirikiana na UNHCR katika kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi lakini pia yapo baadhi ya Mashirika ya Kimataifa yanayoendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza jukumu hilo ikiwemo, Shirika la umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (UNICEF), Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamaji (IOM) na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) na mengineyo.
Mashirika mengine ambayo yaliyoongezeka baada ya ujio wa wakimbizi kutoka Burundi ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula (FAO), Shirika la Kimataifa linalotoa huduma za kijamii (OXFAM), na Shirika la Kimataifa linalohusika na masuala ya watoto na wasiojiweza (PLAN INTERNATIONAL),  Mashirika mengine ni Shirika la Kimataifa la kusaidia wazee (HELP AGE INTERNATIONAL) pamoja na Shirika la Kimataifa la kusaidia watoto (SAVE THE CHILDREN).
Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo ndio inabeba jukumu la Kuwahifadhi na Kuwahudumia Wakimbizi inakabiliana na changamoto mbalimbali za katika kuwahifadhi wakimbizi  ikiwemo Wakimbizi kutoroka katika maeneo yao kwenda kuishi na kufanya kazi na biashara bila vibali kwenye maeneo ya vijiji na mijini ambako kuna fursa nyingi za kimaisha.
Aidha ujio wa wakimbizi umekuwa ukiathiri kwa kiasi kikubwa mazingira, miti imekuwa ikikatwa katika vijiji jirani kwa ajili ya matumizi ya kuni za kupikia na ujenzi wa nyumba za wakimbizi. 
 
Aidha misaada kutoka kwa Mataifa na Mashirika Wahisani imepungua kwa kiwango kikubwa hivyo kusababisha Uhifadhi wa Wakimbizi hapa nchini kukumbwa na ukosefu wa fedha za kutosha na kuathiri upatikanaji wa huduma katika makambi. Huduma zinazoathirika ni pamoja na chakula na kukosekana fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya shule kama madarasa hasa katika kipindi hiki cha ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka nchini Burundi.
 
MWISHO.
 

Back to Top