generica viagra

MASWALI YA WABUNGE WA BUNGE LA 11 LA BAJETI YALIYOJIBIWA NA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Friday, May 12, 2017

 
SWALI NA.129
UJAMBAZI NA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA KATIKA MJI WA BUNDA
MHESHIMIWA ESTER AMOS BULAYA (BUNDA MJINI) Atauliza:-
Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha ndani ya Mji wa Bunda na wahanga wa matukio hayo ni wafanya biashara wadogo wadogo.
Je, ni hatua zipi za kiusalama zimechukuliwa ili kukabiliana na wimbi la ujambazi na unyang’anyi katika Mji wa Bunda.
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA ESTER AMOS BULAYA, MBUNGE WA BUNDA MJINI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa hivi karibuni kulikuwa na wimbi la uhalifu kwa Mkoa wa Mara na Mikoa mingineyo. Jeshi la Polisi limeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali  ya kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu, kadri uchambuzi wa uhalifu unavyo onesha mwenendo na mwelekeo wa uhalifu nchini ukitumika kama zana ya kutabiri uhalifu wa baadaye. Jeshi la Polisi limeendelea kuwajengea uwezo Maafisa, Wakaguzi na Askari kwa kuyatambua na kuyaundia mikakati ya utekelezaji mambo yafuatayo:-
 

 1. Kutabiri mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.
 2. Kuyatambua maeneo nyeti (Hotspots) yenye vivutio vya uhalifu, na kuyapangia ulinzi, misako na doria imara. 
 3. Kuendelea kufanya misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha Ulinzi na Usalama katika maeneo mbalimbali nchini.
 4. Kushirikiana na wadau wote wa Ulinzi na Usalama kubadilishana taarifa za Kiintelijensia pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.

 
Mheshimiwa Spika, Kwa nafasi hii nitoe rai kwa wananchi wote kutoa ushirikiano kwa Jeshi letu la Polisi ili kuwabaini, kuwafichua na kuwakamata ili mkondo wa sheria uchukue nafasi yake kwani hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivi viovu.
 
SWALI NA.150
MAAFISA USALAMA WA KIUME KUWAVUA WANAWAKE NIKABU.
MHESHIMIWA HALIMA ALI MOHAMED (VITI MAALUM) Atauliza:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 19(1) ya Katiba ya Nchi kila mtu anayo haki na uhuru wa kuamini dini aitakayo lakini pia chini ya Ibara ya 15(1)(2) ya Katiba  ni lazima sheria zifuatwe:-
 
Je, ni kwa nini Wanawake wa Kiislamu wapovaa Hijabu Nikabu wanavuliwa na Maafisa Usalama Wanaume.
 
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA HALIMA ALI MOHAMED – MBUNGE WA VITI MAALUM kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Si kweli kuwa Wanawake wa Kiislamu wanapovaa Hijabu Nikabu wanavuliwa na Maafisa Wanaume wa Jeshi la Polisi. Aidha Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza Jeshi hilo, kwa mujibu wa PGO 103(1) ambayo inasema malalamiko yote dhidi ya Polisi lazima taarifa itolewe mara moja kwa Mkuu wa eneo husika na hatua za uchunguzi/upelelezi hufanyika kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Naomba niwaombe wananchi hasusani wanawake pindi wanapofanyiwa vitendo kama hivyo kupeleka malalamiko yao Polisi au kwenye Mamlaka zingine husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
 
SWALI NA. 168
UPATIKANAJI WA BOTI ZA POLISI
MHESHIMIWA HAJI KHATIB KAI (MICHEWENI) Atauliza:-
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeimarisha kwa kuweka boti kwa ajili ya Police Marine maeneo mengi ya Mito, Maziwa na hata Baharini ili kuzuia au kudhibiti ajali zinazopatikana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma katika Mikoa na Wilaya ambazo hazijapata huduma hii.
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA HAJI KHATIBU KAI, MBUNGE WA MICHEWENI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika,  Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma ya boti kwa ajili ya Polisi Wanamaji ili kuzuia na kudhibiti ajali  kwa awamu katika Mikoa au Wilaya ambazo hazijapata huduma  pale uwezo wa kibajeti unapoimarika. Aidha, muda huu ambapo Serikali inaendelea kutafuta fedha hizo huduma hiyo Polisi Wanamaji itatolewa na Vituo vya Wanamaji waliopo karibu kwa kufanya doria maeneo husika.
 
SWALI Na. 168
MASWALI YA NYONGEZA NA MAJIBU.

 1. Ni maeneo yapi nchini ambayo yanapaswa kuwa na huduma za Polisi Wanamaji na Je, kati ya hayo yapi  huduma hizo zipo na wapi hazipo?
 • Maeneo yanayopaswa kuwa na huduma za Polisi Marine ni; Dar Es Salaam, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Tanga, Mara – Shirati,  Mbeya – Kyela, Rukwa -Kipili, Pwani – Mafia, na Lindi. Maeneo ambayo huduma hiyo ipo ni; Dar Es Salaam, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Tanga, Mara – Shirati,  Mbeya – Kipili Kyela. Maeneo ambayo hayana huduma ya Polisi Wanamaji ni Pwani – Mafia na Lindi.
 1. Ni kwa kiasi gani Polisi Wanamaji imeweza kufanikiwa kudhibiti uhalifu wa baharini, maziwani na Mito ikiwemo usafirishaji madawa ya kulevya, magendo, wahamiaji haramu na uvuvi haramu?
 • Polisi Wanamaji imefanikiwa kudhibiti uhalifu kwa kufanya misako na doria na kuweza kufanikiwa kukamata Boti mbili (2) za madawa ya  kulevya toka Iran (Boom), kuwakamata wahamiaji haramu na kuwafiksha idara husika (Uhamiaji) kesi zao zinaendelea Mahakamani na mapambano dhidi ya kuzuia magendo doria zinaendelea kufanyika na kuwakamata wavuvi haramu na kuwafikisha Mahakamani.

 
 

 1. Serikali ina mpango gani wa kuimarisha utendaji wa askari wa kitengo cha Polisi Wanamaji na vifaa?
 • Katika kuimarisha utendaji wa askari wa Polisi Wanamaji, Jeshi la Polisi huwapeleka askari wa kikosi cha maji mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha utendaji wao. Vifaa vya majini vitaendelea kununuliwa kwa kadri ya hali ya uchumi itakavyo imarika pia nchi hisani zimekuwa zikitusaidia upande wa vifaa na mafunzo ikiwemo nchi ya Marekani.
 1. Hali ya Polisi Anga nayo ikoje?
 • Hali ya Polisi Anga ni nzuri kiasi kwani tuna ndege moja ya mabawa ambao ipo matengenezo hapa Dodoma na helikopta mbili ambapo moja ni mbovu  inatengenezwa na hivi karibuni itaanza kazi ya doria angani ili kukabiliana na majanga mengine kama mafuriko, mioto na mengineyo.
 1. Kuna bandari bubu ngapi nchini na zinadhibitiwa vipi?
 • Kuna bandari bubu takribani 150 nchi nzima na hizi zinadhibitiwa kwa askari wa Kikosi cha Polisi Wanamaji kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo hayo.
 1. Serikali imejipanga vipi kudhibiti  ajali za baharini pindi zitakapotokea?
 • Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutoa mafunzo mbalimbali ya uokoaji kwa askari wa kikosi cha majini na kuongeza vifaa vya kusaidia kuokoa maisha pindi ajali ya baharini inapotokea. Aidha, Jeshi la Polisi ni moja ya Taasisi ya kikundi kazi cha Coast Guards ambacho na mambo mengine kitashughulikia ulinzi wa mipaka ya maji ikiwemo na uokoaji.
 1. Ushirikiano kati ya Polisi Wanamaji na vikosi vingine vya wanamaji ukoje? Na nini mafanikio yake?
 • Ushirikiano ni mzuri na hutokea mara panapokuwa na tukio au janga majini, kubadilishana taarifa za kihalifu na mafunzo ya pamoja ili kukabiliana na uhalifu huo. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuzuia magendo, madawa ya kulevya ambapo shehena za madawa na wavuvi haramu wamekamatwa mara kadhaa na kufikishwa Mahakamani.

 
 
SWALI NA.169
MWINGILIANO WA GEREZA NA HOSPITALI YA MKOA IRINGA
MHESHIMIWA ZAINAB NUHU MWAMWINDI (VITI MAALUM) Atauliza:-
Gereza la Wilaya ya Iringa ambalo lipo jirani na Hospitali ya Mkoa wa Iringa limekuwa likisababisha usumbufu kwa wananchi wanaotembea kwa miguu hasa nyakati za usiku.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa mwingiliano wa shughuli za kijamii na shughuli za gereza hilo.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA ZAINAB NUHU MWAMWINDI, MBUNGE WA VITI MAALUM kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ni kweli yalikuwepo malalamiko ya wananchi kupata usumbufu wa kuingia na kutoka Hospitali ya Mkoa wa Iringa ambapo barabara ya kuingia inapita mbele ya lango la Gereza Iringa. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo hasa baada ya kufungwa barabara inayopita mbele ya gereza kuelekea hospitalini kwa watumiaji wa magari, iliukutanisha uongozi wa Manispaa ya Iringa na uongozi wa Jeshi la Magereza Mkoani humo na kutoa maagizo yafuatayo:-

 1. Uongozi wa Manispaa ya Iringa kuandaa barabara mbadala itakayotumiwa na wananchi wanaokwenda hospitalini kwa kutumia gari.
 2. Uongozi wa Manispaa uandae ramani ya ukuta utakaozuia matumizi ya barabara inayopita gerezani kwa kutumia gari. Ukuta huo ulilenga kuzuia magari na kutoa eneo ambalo waenda kwa miguu wangepita bila kuingiliana na shughuli za gereza.
 3. Baada ya kupatikana ramani uongozi wa Magereza ulitakiwa kujenga ukuta huo.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza tayari limekwishatekeleza maagizo hayo kwa kujenga ukuta unaotenganisha barabara ya watembea kwa miguu wanaokwenda hospitali kwa kutumia eneo la mbele ya gereza ili wasiingiliane na shughuli za gereza. Vilevile Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekwisha tekeleza agizo la kujenga barabara mbadala inayotumiwa na wananchi wanaokwenda hospitalini na magari.
Hata hivyo, pamoja na kujengwa barabara mbadala, gereza limeendelea kuruhusu magari yanayokwenda hospitalini kutumia barabara iliyo mbele ya gereza kwa wakati wa dharura.
 
 
SWALI NA. 184
MSAKO WA WAGANGA WA KIENYEJI NCHINI
MHESHIMIWA ELIAS JOHN KWANDIKWA (USHETU) Atauliza:-
Polisi wamekuwa wakifanya msako na kamatakamata ya waganga wa kienyeji sehemu nyingi hapa nchini.

 1. Je, ni waganga wangapi wa kienyeji walikamatwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
 2. Waganga wa kienyeji wangapi walifikishwa Mahakamani na kuwatia hatiani katika kipindi hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA ELIAS JOHN KWANDIKWA, MBUNGE WA USHETU kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Waganga wa kienyeji waliokamatwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ni 26 na kushtakiwa kwa makosa ya kufanya biashara ya uganga bila kibali, kupatikana na Nyara za Serikali.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 jumla ya waganga 16 walikamatwa na kufikishwa Mahakamani, kati ya hao waganga saba (7) walipatikana na hatia kwa kufungwa miaka miwili kila mmoja au kulipa faini ambapo jumla ya watuhumiwa sita (6) katika kesi tofauti walilipa faini ya jumla ya Sh.1,250,000/= Mtuhumiwa wa kesi mmoja (1) alihukumiwa miaka miwili (2) bila yeye kuwepo Mahakamani juhudi za kumsaka zinaendelea.
 
 
SWALI NA.106
SERIKALI KULITUMIA JESHI LA POLISI NCHINI
MHESHIMIWA OTHMAN OMAR HAJI (GANDO) Atauliza:-
Moja kati ya kazi za Polisi ni Ulinzi na Usalama wa raia na mali zao, uzoefu unaonyesha kila zinapotokea kampeni za uchaguzi Jeshi la Polisi hutumika kama Taasisi ya Chama Tawala hivyo husababisha Ulinzi na Usalama (hasa kwa Wapinzani wa Chama Tawala) hutoweka mikononi mwa Polisi:-
Je, Serikali haioni kwamba inalitumia Jeshi la Polisi (ambalo huendesha shughuli zake kwa kodi za watanzania) kwa lengo la kusaidia kudhoofisha Upinzani na kurahisisha kukipatia ushindi chama chake cha CCM.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
 Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA OTHMAN OMAR HAJI, MBUNGE WA GANDO kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ambazo zinatoa mwongozo kwa shughuli za askari.
Mheshimiwa Spika, Naomba ifahamike kwamba Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya Ulinzi wa raia na mali zao na si kwa ajili ya chama fulani cha siasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema. Ni Jeshi linalo watumikia watanzania wote pasipo kujali vyama vyao, kabila zao, dini zao na rangi zao. Hata hivyo, ikitokea askari wamekiuka taratibu za kiutendaji tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kinidhamu dhidi yao pale Wizara yangu inapopata malalamiko rasmi kupitia dawati la malalamiko.
 
MAELEZO YA NYONGEZA 1810

 1. Matukio ya uhalifu yaliyofanywa na wafuasi wa upinzani Zanzibar kabla na baada ya uchaguzi wa marejeo:-
 1. Kuchoma moto na mashamba na nyumba
 2. Kurusha mabomu
 3. Kushiriki katika kuharibu Uchaguzi Mkuu
 4. Kufanya mikusanyiko isiyo halali
 5. Kukashifu viongozi.

Jeshi la polisi lilichukua hatua zifuatazo:

 • Matukio yaliyofanywa na upinzani ni kama mikusanyiko isiyo halali, uchochezi na hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwa kamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na jumla ya watuhumiwa 24 kutoka kusini Pemba na Kaskazini Pemba walishtakiwa ambapo kesi zao ziko katika hatua mbalimbali ikiwemo Mahakamani, DPP, na baadhi zimefungwa katika vituo vya polisi na baadhi ya watuhumiwa wanaendelea kuripoti katika vituo vya polisi.

 
SWALI NA. 34
UTARATIBU WA KUTOA FORM YA PF 3
MHESHIMIWA MWANNE ISMAIL MCHEMBA (VITI MAALUM) Atauliza:-
Form ya PF 3 hutolewa na Polisi tukio linapotokea na kumletea usumbufu mgonjwa kwani anatakiwa kuwa na uthibitisho wa fomu hiyo ili daktari atoe ushauri wake na pia mgonjwa hawezi kupatiwa huduma yoyote mpaka awe na fomu hiyo hata kama ana maumivu makali au hali yake mbaya:-
Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kufanya marekebisho ya utaratibu ili kuwaondolea usumbufu wagonjwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA MWANNE ISMAIL MCHEMBA, MBUNGE WA VITI MAALUM kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka utaratibu wa mtu anapokuwa ameumia apate PF 3 (Police Form 3) kwa mujibu wa Kifungu cha 170 cha Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ili aweze kupokelewa na kupewa matibabu katika hospitali zetu. Msingi mkubwa wa hiyo fomu ni kutaka kujua mazingira ya mtu huyo aliumia wapi na alikuwa anafanya nini.
Mheshimiwa Spika, PF 3 inatumika pia kama kielelezo Mahakamani kama mtu ameshambuliwa ama amepigwa ili Mahakama ijue ameumia kiasi gani na kuwa rahisi kutoa adhabu stahiki. Hata hivyo, kuna matukio mengine yaliyo wazi PF 3 hupelekwa hospitali kwa urahisi wa matibabu, kwa msingi huo PF 3 bado inakidhi matakwa yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Kifungu nilichokitaja hapo juu.
 
 
SWALI NA.98
 
KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI
 
MHESHIMIWA SABREENA HAMZA SUNGURA (VITI MAALUM) Atauliza:-
 
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza ajali za barabarani.
 
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
 
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA SABREENA HAMZA SUNGURA, MBUNGE WA VITI MAALUM kama ifuatavyo:-
 
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa mkakati wa kudhibiti makosa yanayosababisha madhara makubwa (High Risk Factors), ambayo hupelekea ajali za barabarani kuongezeka. Mambo yaliyolengwa katika mkakati pamoja na mambo mengine ni:-
 

 1. Udhibiti wa madereva walevi na kuendesha kwa uzembe, ujahiri na hatari.
 2. Udhibiti wa mwendokasi kwa madereva na wamiliki wa magari, kuwa na madereva wenza kwa mabasi ya safari za zaidi ya masaa manane.
 3. Kudhibiti uendeshaji magari bila sifa/Leseni za Udereva na Bima.
 4. Kudhibiti usafirishaji wa abiria kutumia magari madogo yenye muundo wa tairi moja nyuma kwa mfano; Toyota Noah, Probox n.k.
 5. Kusimamia matumizi ya barabara kwa Makundi Maalum mfano Watoto, Wazee, Walemavu na Wasiotumia vyombo vya moto (mikokoteni na baiskeli).
 6. Kudhibiti ajali za pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na magurudumu matatu.
 7. Kuzishauri Mamlaka husika kuweka alama za kudumu za utambulisho kwenye maeneo hatarishi ya ajali.
 8. Kusimamia utaratibu wa NUKTA (Point System) kwenye Leseni za Udereva.
 9. Marekebisho ya sheria za Usalama Barabarani.
 10. Abiria kufunga mikanda ya usalama wanapotumia vyombo vya usafiri.
 11. Kubaini maeneo tete na hatarishi ya ajali za barabarani (Black  

  Spots/Kilometers).

 1. Kudhibiti utoaji/upokeaji rushwa barabarani.
 2. Motisha kwa askari wanaosimamia vizuri majukumu yao.
 3. Kuwajengea uwezo wa kiutendaji askari wa usalama barabarani.

 
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba suala la Usalama Barabarani siyo la kundi au Taasisi moja tu, ila ni letu sote. Wabunge ni miongoni mwa wahusika wa suala la Usalama Barabarani, kwa maana kuwa nafasi yao kubwa ni katika kuuelimisha umma na kusaidia katika ujenzi wa utamaduni wa kuheshimu alama za Usalama Barabarani nchini.
 
SWALI NA.151
KUWEKA KITUO CHA UHAMIAJI KATIKA MPAKA WA TANZANIA NA MSUMBIJI
MHESHIMIWA DAIMU MPAKATE (TUNDURU KUSINI) Atauliza:-
Katika upande wa Kusini mwa Jimbo la Tunduru Kusini wananchi takribani 200 wa Tanzania na Msumbiji huvuka mto Tuvuma kila siku kutafuta mahitaji yao ya kila siku, upande wa Msumbiji wameweka Askari wa Uhamiaji ambao huwanyanyasa sana watanzania kwa kuwapiga na kuwanyang’anya mali zao kwa kukosa hati ya kusafiria.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Kituo cha Uhamiaji katika Kijiji cha Makando, Kazamoyo na Wenye ili kuwapatia Watanzania huduma ya Uhamiaji.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA DAIMU MPAKATE, MBUNGE WA TUNDURU KUSINI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha kuwa inasogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za Uhamiaji. Katika kutekeleza hilo Wilaya zilizo nyingi ikiwemo Tunduru zina Ofisi za Uhamiaji. Aidha Serikali inatambua umbali mrefu (kama 90 Kms) uliopo kutoka Vijiji vya Makando, Kazamoyo na Wenye kutoka Mjini Tunduru zilipo Ofisi za Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua hilo na uhitaji wa huduma za Uhamiaji katika Vijiji hivyo ili kuwawezesha Wanakijiji kuingia na kwenda nchini Msumbiji kihalali tunafanya ufuatiliaji ili kujua gharama za kufungua Ofisi ya Uhamiaji katika Kijiji cha Makando kwa kuanzia. Ofisi hiyo itahudumia Vijiji vya Kazamoyo na Wenye ili kuwawezesha kuvuka mpaka kihalali. Tunawaomba wananchi na Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwa kuzingatia kuwa suala hili linahitaji kutengewa fedha katika bajeti.
 
 
SWALI NA. 51
MAGARI YA ZIMAMOTO MKOA WA KILIMANJARO
MHESHIMIWA RAPHAEL JAPHARY MICHAEL (MOSHI MJINI) Atauliza:-
Mkoa wa Kilimanjaro una tatizo la uhaba wa magari ya Zimamoto. Gari linalofanya kazi mpaka sasa ni moja tu hivyo kufanya huduma ya Zimamoto kuwa duni sana.

 1. Je, ni lini Serikali itaongeza magari mengine mawili ili kusaidia shughuli za Zimamoto na kuepusha hasara zinazowakabili wananchi wanaopata majanga ya moto;
 2. Je, Serikali haioni kwamba uamuzi wa kuhamishia Kitengo cha Zimamoto Wizara ya Mambo ya Ndani kumeiongezea mzigo Wizara hiyo na kupunguza ufanisi wa shughuli za Zimamoto.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Napenda kujibu swali la MHESHIMIWA RAPHAEL JAPHARY MICHAEL, MBUNGE WA MOSHI MJINI lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ni kweli kwamba Mkoa wa Kilimanjaro una gari moja kubwa la kuzima moto ambalo lina uwezo wa kubeba maji lita 7000 na madawa ya kuzimia moto wa mafuta lita 400. Aidha, kwa sasa kuna magari mawili madogo ya kuzimia moto yasiyo na matanki ya kubeba maji na madawa. Magari haya hufanya kazi kwa kupata maji kutoka gari lingine au kutoka katika vituo maalum vya maji ya Zimamoto (Fire Hydrant). Hata hivyo, kwa sasa ni gari moja tu linalofanya kazi na jingine ni bovu.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kununua magari mapya ya Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali inafanya mazungumzo na Taasisi mbalimbali za nje ya nchi ambazo zimeonyesha nia ya kutukopesha fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya Zimamoto na Uokoaji na pindi mazungumzo hayo yatakapokamilika mikataba itasainiwa ili magari hayo yaanze kutengenezwa.
Mheshimiwa Spika, Kuhamishwa kwa Kitengo cha Zimamoto kutoka katika Mamlaka mbalimbali na kuwekwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kulifanywa baada ya tathimini kufanyika kuhusiana na utendaji wa kazi za kila siku, ambapo ilibainika kuwa utendaji kazi wa Vikosi vya Zimamoto katika Halmashauri ulikuwa dhaifu kutokana na vikosi hivyo kuwa chini ya Wahandisi wa Majiji, Manispaa na Miji, ambao hawakuwa wataalam wa masuala ya Zimamoto na Uokoaji. Aidha, ilibainika pia vikosi vilivyokuwa chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vihamishiwe Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuleta ufanisi zaidi wa kazi na viwe chini ya Kamandi moja ili viweze kupokea amri kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba uamuzi huo umeongeza ufanisi na sio mzigo.
 
MAELEZO YA NYONGEZA

 1. Je, ni Kampuni gani ambazo kwa sasa Serikali ipo kwenye mazungumzo nazo kwa ajili ya kukopeshwa fedha za kununulia mitambo ya kuzimia moto.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ipo katika mazungumzo na REIFEISEN BANK ya Austria itatoa kiasi cha Euro Milioni 5 na KCB BANK ya Ubelgiji Euro Million 19 hii itasaidia ununuzi wa magari ya Zimamoto na Uokoaji.

 1. Nini kauli ya Serikali juu ya ununuzi wa magari mengi ya washawasha kwa gharama kubwa wakati Serikali hiyo hiyo imeshindwa kununua hata magari mawili ya kuzimia moto kwa kila Mkoa.

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeamua katika mazungumzo kati ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa magari ya washa washa yatumike katika shughuli za Zimamoto na Uokoaji katika Mikoa yote Tanzania Bara.

 1. Inaonekana magari mengi ya kuzimia moto yaliyopo katika baadhi ya Mikoa ni mabovu na hayafanyiwi matengenezo. Je, kwa nini sasa Serikali isione haja ya kurudisha huduma hiyo kwenye Mamlaka za Halmashauri, Miji na Majiji kwa Serikali Kuu imeshindwa kutoa huduma hiyo kikamilifu.

Sheria Namba 14 ya mwaka 2007 iliyounda Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ilikuwa na lengo kuu la kuviunganisha vikosi vyote vya Zimamoto na Uokoaji Tanzania Bara na kuwa chini ya Kamandi moja ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuongeza ufanisi na muungano wa kikazi baina ya viwanja vya ndege, bandari na halmashauri za Miji ili kutimiza lengo la uokoaji.
 
SWALI NA.33
AJALI YA BODABODA
MHESHIMIWA ABDALLAH HAJI ALI (KIWANI) Atauliza:-
Usafiri wa bodaboda unatoa ajira kwa vijana walio wengi na kurahisisha usafiri lakini zimekuwa zikisababisha ajali nyingi mara kwa mara.
Je, ni watu wangapi wamepoteza maisha na wangapi wamejeruhiwa na ajali za pikipiki kuanzia mwaka 2010 hadi 2017?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Atajibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la MHESHIMIWA ABDALLAH HAJI ALI, MBUNGE WA KIWANI kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Pikipiki za matairi mawili (Bodaboda) na matairi matatu (Bajaji) zilianza kutumika kubeba abiria kuanzia mwaka 2008. Mwaka 2010 Serikali ilipitisha kanuni na masharti ya usafirishaji wa Pikipiki. Aidha, katika kipindi hicho hakukua na utaratibu wowote wa kusimamia biashara ya waendesha pikipiki wanaobeba watu.
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2010 hadi Februari, 2017 kumekuwa na jumla ya ajali 31,928 zilizosababisha vifo vya watu 6,529 na majeruhi 30,661.
 
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI - WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI.
 
 
 
 
 

Back to Top