generica viagra

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. MWIGULU LAMECK NCHEMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2017/18

Tuesday, May 9, 2017

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. MWIGULU LAMECK NCHEMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2017/18
 

 1. UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu, baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2016/17 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2017/18.

 

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuwasilisha Hotuba hii kwa mara ya kwanza nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua kuwa Waziri katika Wizara hii nyeti inayosimamia usalama wa nchi. Naahidi kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuhakikisha kuwa hali ya usalama nchini inaendelea kuimarika ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Job Y. Ndungai (Mb.) pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kwa kuendesha na kusimamia vema shughuli za Bunge. Pia, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maoni yao yanayolenga kuboresha utendaji wa Wizara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kwa kuyachambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka 2017/18. Naishukuru Kamati hiyo kwa maelekezo, ushauri na maoni yanayolenga katika kuboresha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kutoa pole kwa familia na wananchi kwa ujumla kutokana na vifo, ulemavu, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu vilivyosababishwa na matetemeko ya ardhi, mafuriko, ajali za barabarani, majini na nchi kavu katika kipindi chote kutoka mwezi Julai, 2016 hadi Machi, 2017.

 

 1.  HALI YA USALAMA NCHINI

 

 1. Mheshimiwa Spika, moja ya wajibu mkubwa na muhimu wa Serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo nchini. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeendelea kutekeleza wajibu huo kwa kusimamia sheria; kupambana na kudhibiti uhalifu wa aina zote unaoweza kuathiri hali ya amani na utulivu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hali ya usalama nchini imeendelea kuwa tulivu licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali kama ongezeko la vyombo vya moto (pikipiki na magari), utandawazi, kuongezeka kwa watu mijini, kuongezeka kwa mbinu za uhalifu, migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likikabiliana nayo. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 kulikuwa na matukio makubwa ya uhalifu wa jinai 56,913 ambapo makosa 53,850 yaliripotiwa kutoka Tanzania Bara na mengine 3,063 yaliripotiwa kutoka Zanzibar.

 

 1. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha makosa hayo yameongezeka kwa asilimia 7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2015/16. Ongezeko hilo linatokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukuaji wa miji, utandawazi na kuongezeka kwa mbinu mpya za uhalifu. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vya ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi ili kuhakikisha hali ya usalama na utulivu inaendelea kudumishwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, makosa makubwa ya jinai yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni makosa dhidi ya binadamu, makosa ya kuwania mali na makosa dhidi ya maadili ya jamii. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi nchini yalikuwa kama ifuatavyo: makosa dhidi ya binadamu 10,089; makosa ya kuwania mali 29,476; na makosa dhidi ya maadili ya jamii yalikuwa 17,348. Aidha, jumla ya watuhumiwa 52,353 wa makosa makubwa ya jinai walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria, misako, kushirikisha jamii na kutoa elimu kwa umma ya namna ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mauaji ni mojawapo ya makosa dhidi ya binadamu yanayoendelea kutokea kutokana na sababu mbalimbali. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya matukio 2,470 ya mauaji yalitokea na watu 2,532 waliuawa ambapo wanaume ni 2,067 na wanawake 465. Idadi kubwa ya mauaji ilijitokeza kwenye matukio yaliyohusisha wizi wa mifugo, ujambazi, imani za kishirikina, wivu wa kimapenzi, unyang’anyi wa pikipiki na magari pamoja na ulevi. Matukio hayo yalijitokeza kwa wingi katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Mbeya na Tabora. Upelelezi wa kesi hizi unaendelea na watuhumiwa 1,619 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na uhalifu huo pamoja na kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 silaha 410 na risasi 2,262 zilikamatwa kwa mchanganuo ufuatao: gobore 217 na risasi 361; shotgun 62 na risasi 386; FN 8, bastola 49 na risasi 403; Sub Machine Gun (SMG) 27 na risasi 1,025; Semi Automatic Rifle (SAR) moja (1) na risasi 9; Mark iv 12 na risasi 33, Rifle 32 na risasi 31; risasi 14 za G3 na AK47 mbili (2). Aidha, kulikuwa na matukio 576 ya ujambazi wa kutumia silaha yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi nchini katika kipindi hicho. Matukio hayo yalijitokeza kwa wingi katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Morogoro, Mara, Mwanza, Shinyanga na Tabora, Mikoa ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Tarime – Rorya. Watuhumiwa 306 waliopatikana na silaha haramu walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 24 Januari, 2017 Jeshi la Polisi liliteketeza jumla ya silaha 5,608 zilizosalimishwa na nyingine zilizopatikana katika mazingira ya uhalifu kuanzia mwaka 2013 hadi 2016. Miongoni mwa silaha zilizoteketezwa ni pistol - 21, toy pistol - 21, shotgun - 606, rifle - 300, gobore - 4,487, SMG - 166, G3 - 01, FN rifle - 03 na SAR - 03. Aidha, nachukua nafasi hii kuhimiza wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe kwenye vituo vya Polisi au Ofisi za Watendaji wa Kata na Vijiji. Katika mwaka 2017/18 Jeshi litaendelea kufanya doria, misako na operesheni za mara kwa mara kwa lengo la kuwabaini waingizaji na watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria ili kudhibiti vitendo vya uhalifu nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na wimbi la umiliki haramu wa silaha nchini Jeshi la Polisi lilianzisha zoezi la uhakiki wa silaha mwezi Machi, 2016 ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2017 asilimia 63.20 ya silaha zilizosajiliwa zilikuwa zimehakikiwa. Katika zoezi hilo jumla ya silaha 486 zilisalimishwa kutokana na kutomilikiwa kihalali ambazo ni pistol - 16, rifle - 18, shotgun - 161, SMG - 24, G3 - 1 na magobore 266 katika mikoa mbalimbali nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeongeza muda wa uhakiki mpaka tarehe 30 Juni, 2017 ili kutoa nafasi kwa wamiliki wa silaha ambao hawakupata nafasi ya kuhakiki silaha zao kwa muda uliotolewa awali. Natoa rai kwa wamiliki wa silaha kuhakiki silaha zao kwa muda uliopangwa vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zao za kumiliki silaha.

 
Hali ya Usalama Barabarani
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya matukio 6,500 ya usalama barabarani yaliripotiwa nchini. Katika matukio hayo jumla ya ajali 1,552 zilisababisha vifo vya watu 2,372 na watu 6,074 kujeruhiwa. Takwimu zinaonesha kupungua kwa ajali hizo kwa asilimia 7 kwani katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16 kulikuwa na jumla ya ajali za barabarani 7,006 zilizoripotiwa ambapo watu 2,589 walipoteza maisha na watu 7,536 walijeruhiwa. Kwa ujumla ajali nyingi kati ya hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva, kutozingatia sheria za usalama barabarani, mwendo kasi, ulevi pamoja na ubovu wa magari na miundombinu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia sheria za usalama barabarani ambapo kwa kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya madereva 6,500 wa magari mbalimbali na waendesha pikipiki 5,865 ambao walikamatwa na kupelekwa mahakamani kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti vyanzo vya ajali za barabarani kwa kushirikiana na wadau wengine kama Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Shule za Udereva zilizosajiliwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: kuongeza idadi ya askari wa usalama barabarani; kuendeleza zuio la magari ya abiria kusafiri baada ya saa 4 usiku; kudhibiti mwendo kasi kwa kuweka vituo vya ukaguzi wa ratiba za magari ya abiria; kuimarisha doria na ukaguzi wa magari barabarani; kufuta leseni za madereva wanaosababisha ajali kubwa; kuzuia leseni kwa kipindi maalum kwa madereva wanaofanya makosa madogo; kutoa elimu ya usalama barabarani kwa njia za redio na luninga kwa madereva na jamii yote; na kuhakikisha wamiliki wa vyombo vya usafiri wanaajiri madereva wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia sheria za usalama barabarani na kuelimisha jamii kuzingatia sheria na taratibu hizo.

 

 1. UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA MHE. RAIS WA AWAMU YA TANO

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoyatoa tarehe 20 Novemba, 2015 kupitia hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa Bunge la 11 pamoja na maelekezo mengine aliyoyatoa kwa nyakati tofauti kama ifuatavyo:

 
Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya kilogramu 16 na gramu 223 za cocaine pamoja na kilogramu 37 na gramu 118 za heroine zilikamatwa na watuhumiwa 1,241 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Aidha, katika kipindi hicho kilo 36,337 na gramu 426.76 za bangi zilikamatwa na watuhumiwa 12,691 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa sasa operesheni mbalimbali za kupambana na uingizaji, usambazaji na ulimaji wa bangi zinaendelea nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola pamoja na raia wema. Aidha, Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na Mashirika ya Kimataifa katika kubaini waingizaji na wasambazaji wa dawa za kulevya nchini.

 
Kutatua Tatizo la Wananchi Kubambikizwa Kesi
 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua stahiki za kukabiliana na malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi zimechukuliwa, ambapo Wizara kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kupokea malalamiko na kuyashughulikia. Malalamiko hayo yameendelea kupokelewa katika Ofisi za Wakuu wa Polisi za Wilaya na Mikoa pamoja na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Jeshi la Polisi limepokea malalamiko 206, ambapo malalamiko 203 ni ya kutoka kwa wananchi na malalamiko matatu (3) ni ya ndani ya Jeshi. Takwimu zinaonesha ongezeko la malalamiko 138 ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka 2015/16, ambapo kulikuwa na jumla ya malalamiko 68, kati ya hayo, malalamiko 64 yalitoka kwa wananchi na malalamiko manne (4) yalikuwa ni ya ndani ya Jeshi la Polisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi lilichukua hatua mbalimbali za kinidhamu kwa watendaji ambao walifanya makosa hayo kwa kuwafukuza kazi askari 14 na maafisa wawili (2); kuwashusha vyeo askari wanne (4); na askari sita (6) walipewa adhabu nyingine.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeimarisha utaratibu na usimamizi wa utendaji katika kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayofikishwa vituoni kwa kutoa miongozo mara kwa mara kwa wakuu wa vituo na wakuu wa upelelezi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, miongozo hiyo ni pamoja na: kusimamia kwa karibu upelelezi wa mashauri yote kabla ya kuyapeleka kwa wanasheria wa Serikali; kushirikiana kwa pamoja kati ya wapelelezi na waendesha mashtaka kutoka hatua za awali za upelelezi mpaka hatua ya mwisho wa kesi mahakamani; na kuendelea kusimamia na kudhibiti vitendo vya utovu wa nidhamu na ukiukaji wa maadili vinavyofanywa na baadhi ya wapelelezi kwa kuweka mfumo maalum wa kupokea taarifa za siri kutoka kwa wananchi juu ya wapelelezi wasio waadilifu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na miongozo hiyo, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa askari juu ya madhara ya kuwabambikia kesi wananchi, imeimarisha ushirikiano na wananchi kwa kufanya vikao nao ili kuwajengea imani waweze kutoa taarifa kwa viongozi pale wanapofanyiwa vitendo wasivyoridhika navyo, pia imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa Haki Jinai na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka katika hatua mbalimbali za mashauri ya jinai na inaendelea kuimarisha vitengo vya ukaguzi kuanzia ngazi ya Makao Makuu ya Polisi, Mikoa, Wilaya na Vituo ili kubaini ubambikizwaji wa kesi kwa wananchi. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia na kufuatilia nidhamu ya askari ili kuwa na watendaji wenye weledi.

 
Upandishwaji Vyeo kwa Askari
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara inapandisha vyeo askari kutokana na sifa na muundo wake wa kiutumishi. Mapendekezo ya upandishwaji vyeo yameendelea kuzingatia uwepo wa nafasi, bajeti, sifa binafsi kama inavyobainishwa katika miuundo na elimu kuwa kigezo cha ziada. Katika mwaka 2016/17, jumla ya askari 4,604 walipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali ambapo askari 4,137 ni wa Jeshi la Polisi na askari 467 ni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

 
Malipo ya Madai ya Askari
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuepuka ucheleweshwaji wa malipo ya madai ya askari, Serikali imelipa madeni ya watumishi jumla ya Shilingi 14,872,010,390 kwa mwaka 2016/17 kwa mchanganuo ufuatao: Jeshi la Polisi Shilingi 6,205,212,689.14; Jeshi la Magereza Shilingi 7,510,430,711; Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Shilingi 751,869,659.36; na Idara ya Uhamiaji Shilingi 404,497,330. Madeni hayo ni ya kipindi cha mwaka 2014/15 ambayo yalitokana na malimbikizo ya posho za likizo na safari za kikazi ndani na nje ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Polisi limeimarisha Kitengo cha Uhasibu kwa kuongeza watendaji na lina mipango ya kuanzisha kanda za malipo (Payroll Points) ili kuhakiki madai ya askari kwa haraka. Hadi kufikia mwezi Januari, 2017 askari wapya 3,164 wote walikuwa wamelipwa mishahara yao na malimbikizo ya posho zao za chakula ambazo hawakuwa wamelipwa tangu waanze kazi. Pia, suala la mapunjo ya mishahara ya watumishi yanayotokana na watumishi/askari kupandishwa vyeo limeanza kushughulikiwa kwa awamu baada ya zoezi la uhakiki wa watumishi kukamilika.

 
Kuzingatia Sheria katika Kutoa Hati za Uraia
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji imeandaa na kusambaza mwongozo unaotoa ufafanuzi kuhusu Sheria ya Uraia Na. 6 ya Mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002, pamoja na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu uraia wa watu wanaotiliwa mashaka. Aidha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetoa tafsiri ya uraia wa Tanzania kwa kuzaliwa na hivyo kuondoa mkanganyiko uliokuwepo.

 
Vibali vya Kuishi Nchini kwa Wageni
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu imeendelea kusimamia Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016, ili kutatua changamoto za kiutendaji zinazojitokeza katika utoaji wa vibali vya kazi na ukaazi. Aidha, Wizara imeandaa utaratibu maalum wa kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa vibali vya ukaazi vinavyotolewa.

 
Utekelezaji wa Mpango wa Kuhamia Dodoma
 

 1. Mheshimiwa Spika, kufuatia agizo la Mhe. Rais la tarehe 23 Julai, 2016 la kuhamishia Makao Makuu ya Serikali katika Mji wa Dodoma, Wizara imewahamisha jumla ya watumishi 45 katika awamu ya kwanza. Aidha, watumishi wengine wataendelea kuhama kulingana na   mpango uliopo. Katika bajeti ya maendeleo ya mwaka 2017/18 jumla ya Shilingi 4,700,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa ofisi kama ifuatavyo: Jeshi la Polisi Shilingi 100,000,000, Jeshi la Magereza 2,200,000,000, Idara ya Uhamiaji Shilingi 200,000,000 na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Shilingi 2,200,000,000.

 
 

 1. MAPITIO YA BAJETI YA MWAKA 2016/17, UTEKELEZAJI WA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) PAMOJA NA MALENGO YA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2017/18

 
   Mapato na Matumizi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Wizara iliendelea kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopangwa. Katika kutekeleza majukumu hayo, Wizara iliidhinishiwa na Bunge jumla ya Shilingi 867,190,349,608.87. Kati ya fedha hizo, Shilingi 47,923,421,105 zilikuwa ni za miradi ya maendeleo, Shilingi 500,056,492,105 zilikuwa kwa ajili ya mishahara na Shilingi 319,210,436,398.87 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo kwa Wizara na Taasisi zake.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2017 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 644,862,980,215.64 sawa na asilimia 74 ya bajeti yote. Kati ya fedha hizo, Shilingi 13,466,336,364 zilikuwa ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, sawa na asilimia 28 ya bajeti ya maendeleo, Shilingi 366,462,364,559 zilikuwa ni Mishahara na Shilingi 264,934,279,292.64 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Pia, Wizara ilikusanya jumla ya Shilingi 178,339,863,952.10 ikiwa ni maduhuli sawa na asilimia 62 ya lengo la Shilingi 289,946,031,504.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi 293,822,132,859. Ili kufikia lengo hilo, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato pamoja na kutumia mifumo ya kieletroniki.

 
Kuliongezea Jeshi la Polisi Rasilimali Watu na Rasilimali Fedha
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Wizara kupitia Jeshi la Polisi imeajiri jumla ya askari wapya 3,164 kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi. Ajira hizi ni katika kutekeleza  Ibara ya 146 (i) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 inayoelekeza Serikali kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuviongezea rasilimali watu na rasilimali fedha.

 
Maslahi ya Watendaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watendaji wa vyombo vya usalama kwa kuwapatia ration allowance za kila mwezi kwa wakati kama Ibara ya 146 (ii) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 inavyoelekeza. Aidha, Serikali imeanza kuwapatia askari wa Jeshi la Polisi fedha ya msamaha wa kodi kwa mwezi. Katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya maslahi ya watendaji wa vyombo vya usalama ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

 
Kushiriki katika Kuimarisha Amani na Usalama katika Nchi Mbalimbali
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ibara ya 146 (iv) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020, Wizara inashiriki katika majukumu ya kiusalama na amani kwenye nchi mbalimbali kwa kupeleka askari wake. Lengo likiwa ni kuwezesha majeshi yetu yaendelee kupata uzoefu na mbinu za kisasa. Katika mwaka 2016/17, jumla ya askari 102 wa Jeshi la Polisi wanashiriki katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa katika nchi mbalimbali, ambapo Sudan - Darfur kuna askari 87, Sudan - Abyei askari sita (6), Sudani Kusini askari wawili (2), Marekani – New York askari mmoja (1) na Lebanon askari sita (6).

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, jumla ya maafisa 155 walifaulu mtihani wa usaili uliofanyika tarehe 20 Februari, 2017 na wanasubiri kwenda kushiriki majukumu hayo nje ya nchi. Kwa upande wa Jeshi la Magereza wapo askari wawili (2) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanne (4) Sudan Kusini.

 
Usalama wa Makundi Maalum na Ulinzi Shirikishi
 

 1. Mheshimiwa Spika, Ibara 146 (v) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 –2020, pamoja na mambo mengine inaelekeza kutoa elimu kwa umma dhidi ya imani potofu zinazosababisha mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya watu 164 waliuawa, kati ya hao wanawake ni 96 na wanaume 68. Matukio hayo yalitokea Mikoa ya Geita 7, Iringa 4, Kagera 5, Kigoma 12, Mbeya 4, Mwanza 13, Njombe 17, Rukwa 5, Shinyanga 11, Simiyu 5, Singida 3, Songwe 21 na Tabora 57. Kufuatia matukio hayo watuhumiwa 161 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi pia limeendelea kuimarisha mpango wa ulinzi shirikishi na kushirikiana na wadau mbalimbali nchini katika kutoa elimu kwa umma kuhusu imani potofu zinazosababisha mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino. 

 

 1. Mheshimiwa Spika, hatua kali za kisheria zimeendelea kuchukuliwa kwa wote wanaobainika kujihusisha na uhalifu wa aina hii. Napenda kutoa taarifa kupitia Bunge hili kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2017 hapakuwa na tukio lolote la mauaji au kujeruhiwa lililoripotiwa kuhusiana na vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kudhibiti na kuzuia mauaji ya wazee, watu wenye ualbino na makundi mengine maalum ili kudhibiti vitendo hivyo nchini. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kuacha mila, desturi na imani potofu zinazosababisha madhara kwa makundi hayo.

 
Kushirikiana na Mataifa Mengine na Asasi za Kimataifa katika Kupambana na Uhalifu
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na Mataifa mengine na vyombo vingine vya kimataifa vikiwemo Shirika la Polisi la Kimataifa (INTERPOL) na Mashirika ya Kipolisi ya Kanda za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SARPCCO na EAPCCO) kama Ibara 146 (vi) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 inavyoelekeza katika kupambana na makosa yanayovuka mipaka. Katika mwaka 2016/17, Wizara kupitia Jeshi la Polisi imefanya operesheni za pamoja na nchi za SARPCCO na EAPCCO ambapo jumla ya watuhumiwa 193 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na wote wamefikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kupambana na kudhibiti uhalifu wa aina zote ikiwemo makosa yanayovuka mipaka kwa kushirikiana na mataifa mengine na asasi za kimataifa pamoja na kufanya doria, misako na operesheni maalum za mara kwa mara za nchi kavu na majini.

 
Kuboresha Makazi kwa Askari
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya makazi ya askari, Wizara imeendelea kutekeleza miradi ya ukarabati na ujenzi wa nyumba katika mikoa mbalimbali. Kwa upande wa Jeshi la Polisi miradi ifuatayo ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari inaendelea katika mikoa ya: Njombe (Ludewa) familia 12; Mara (Musoma) familia 24; Mwanza (Mabatini) familia 24; na Kagera (Buyekera) familia 12. Aidha, hatua za awali zinaendelea kwa ajili ya maandalizi ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya familia 4,136 za askari na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza katika mwaka 2017/18.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jeshi la Magereza kazi za ujenzi wa block 12 za magorofa kwa ajili ya familia 320 za askari umeanza kwa kukamilisha ujenzi wa misingi ya block zote na kazi ya kupandisha kuta inaendelea. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 jumla ya Shilingi 5,000,000,000 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi huo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha kuwa fedha hizo zimetolewa ili kuboresha makazi ya askari. Katika mwaka 2017/18, Jeshi la Magereza litaendelea na ujenzi wa nyumba hizo pamoja na kuanza ujenzi wa nyumba 50 za makazi ya askari katika Gereza Isanga – Dodoma.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Idara ya Uhamiaji inaendelea kujenga ofisi, ambapo katika Mkoa wa Pwani ujenzi umefikia asilimia 97 na kazi inayofanyika kwa sasa ni kumalizia kazi za nje. Aidha, ujenzi wa nyumba ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza umefikia asilimia 94 na Mkandarasi anavuta umeme pamoja na kazi za kumalizia (finishing phase).  Kazi nyingine iliyofanyika ni ujenzi wa nyumba ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma ambao umefikia asilimia 92 na Mkandarasi anamalizia kazi ndogo ndogo. Katika Mkoa wa Lindi mradi umefikia asilimia 76 na kazi inayofanyika kwa sasa ni kuweka mifumo ya umeme, TEHAMA na viyoyozi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, miradi mingine inayoendelea chini ya Idara ya Uhamiaji ni kama ifuatavyo: Mkoa wa Geita mradi umefika wastani wa asilimia 50 na kazi inayofanyika kwa sasa ni kuweka paa; Mkoa wa Mtwara mradi umeendelezwa kwa asilimia 23 na kazi inayofanyika kwa sasa ni kumwaga jamvi la ghorofa ya pili; ujenzi wa nyumba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji katika eneo la Masaki – Dar es Salaam upo katika wastani wa asilimia 65 na kazi inayofanyika kwa sasa ni kupiga plasta; na ujenzi wa nyumba tano (5) za Makamishna wa Uhamiaji Mtoni Kijichi (Dar es Salaam), ambapo mkandarasi anafanya kazi za nje na kuweka umeme na maji. Katika mwaka 2017/18 Idara ya Uhamiaji itaendelea kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi wa makazi kulingana na upatikanaji wa fedha.

 
Miradi ya Ujenzi wa Ofisi na Vituo vya Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea na ujenzi wa vituo vya Polisi katika Mikoa ifuatayo: Kituo cha Polisi Daraja A Ludewa, Njombe kimefikia asilimia 60; Kituo cha Polisi Daraja B Mkokotoni, Unguja (asilimia 60); Kituo cha Polisi Daraja C Mtambaswala, Nanyumbu Mtwara (asilimia 85); na Kituo cha Polisi Daraja B Newala, Mtwara (asilimia 85).

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi linaendelea na ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya, Rungwe na Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya, Chunya ambayo imetekelezwa kwa asilimia 80; ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja B Mbweni – Dar es Salaam (asilimia 80); ujenzi wa Kituo cha Polisi Madale – Dar es Salaam (asilimia 95); na ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja C Kiluvya – Dar es Salaam (asilimia 55). Natumia nafasi hii kuwashukuru wananchi wa maeneo husika kwa kujitolea kwao katika ujenzi wa ofisi na vituo hivyo vya Polisi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali (Police Force Corporation Sole) linaendelea na kazi zifuatazo: ujenzi wa Kituo Kipya cha Polisi Daraja A Oysterbay – Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 92; ujenzi wa nyumba 23 za makazi ya maofisa wa juu wa Polisi – Mikocheni ambao umekamilika kwa asilimia 95; na ujenzi wa nyumba za familia 330 Kunduchi, Dar es Salaam ambao umekamilika kwa asilimia 86.

 
 
Upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi
 

 1. Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2017 Serikali ilisaini mkataba na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi. Mkataba huo ni msaada ambao utawezesha ujenzi wa majengo matatu (3) yenye madarasa 13 na kuweza kuchukua wanafunzi 500, ofisi sita (6) na mabweni manne (4) yenye uwezo wa kuishi wanafunzi 300. Mkandarasi Kampuni ya Jiang Su Jiang Du Construction Group Limited imeanza maandalizi ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika Julai, 2019.

 

 1. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo ya utekelezaji wa jumla wa Wizara, maeneo mengine yaliyotekelezwa kupitia Idara Kuu ambazo ni Jeshi la Polisi (Fungu 28), Jeshi la Magereza (Fungu 29), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Fungu (14), Idara ya Uhamiaji (Fungu 93) na Makao Makuu ya Wizara inayojumuisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Fungu 51 ni kama ifuatavyo:

 
JESHI LA POLISI
 
Udhibiti wa Uhalifu Nchini
 

 1. Mheshimiwa Spika, usalama wa raia na mali zao umeendelea kudumishwa kwani ni nguzo muhimu katika maendeleo ya Taifa na maendeleo ya wananchi. Katika mwaka 2016/17, Jeshi la Polisi linaendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu kupitia doria, misako na oparesheni maalum zilizofanyika nchi nzima.

 
Kuanzisha Mkoa Mpya wa Kipolisi Rufiji
 

 1. Mheshimiwa Spika, matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yenye kuhusiana na mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi pamoja na uporaji wa silaha yameendelea kujitokeza katika Mkoa wa Pwani, hususan katika Wilaya ya Kibiti. Itakumbukwa tarehe 13 Aprili, 2017 katika eneo la Mkenge Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani askari nane (8) waliokuwa kazini waliuawa baada ya kushambuliwa na kundi la majambazi wenye silaha. Katika tukio hilo askari mmoja alijeruhiwa na silaha nne (4) aina ya SMG na Long range tatu (3) ziliporwa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, uvamizi wa askari waliopo kazini na kuuawa ni muendelezo wa matukio yaliyowahi kutokea katika vituo vya polisi, malindo na baadhi ya benki. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama itaendelea kuwabaini wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo haramu pamoja na washirika wao ili kuwachukulia hatua stahiki za kisheria.

 

 1. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama haitafumbia macho matukio ya aina hiyo na itahakikisha kuwa watuhumiwa wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria. Nawaomba wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za wahalifu na uhalifu ili kuendelea kudumisha amani na usalama nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko la matukio makubwa ya uhalifu katika Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji katika mwaka 2017/18 Serikali inatajaria kuanzisha Mkoa Mpya wa Kipolisi Rufiji ili kusogeza huduma ya polisi karibu zaidi na wananchi na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo. Wilaya ya Mafia nayo itakuwa ndani ya Mkoa huo mpya.

 
Utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Jeshi la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Usalama wa Jamii (Community Safety Initiave - CSI) kwa kuanzia na Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni. Mpango huo ni wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2018/19 na umelenga katika maeneo makuu manne ambayo ni: kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa polisi; kuboresha utoaji wa huduma; kuboresha mawasiliano na ushirikishwaji wa jamii katika utendaji wa polisi; na utafutaji wa rasilimali kutoka vyanzo mbalimbali.   

 

 1. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango huo ni kuwa na Vituo vya Polisi vinavyohamishika vitatu (3) katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha uhalifu ambayo ni Masaki, Oysterbay na Manzese. Lengo la vituo hivyo ni kuwawezesha askari kufika katika sehemu za matukio kwa haraka. Aidha, kituo cha kisasa cha miito ya mawasiliano (Call Centre) katika Mkoa wa Dar es Salaam kimeimarishwa na kinawarahisishia wananchi kutoa taarifa za matukio na kuwawezesha askari kufika katika eneo la tukio ndani ya dakika 15.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ya mpango huo ni kufungwa kwa vifaa maalumu (Global Position System - GPS) katika magari yote ya Polisi ya Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kwa ajili ya kudhibiti na kufuatilia wahalifu na uhalifu. Maboresho hayo yanatarajiwa kuanza kutekelezwa nchi nzima kwa kuanzia na mikoa yenye matukio makubwa ya uhalifu ambayo ni Arusha, Dodoma, Geita na Mwanza pamoja na Mikoa ya Kipolisi ya Ilala na Temeke.

 
Kudhibiti Uvunjifu wa Amani Unaotokana na Migogoro ya Wakulima na Wafugaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Polisi limendelea kushirikiana na Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuzuia mauaji, kujeruhi na uharibifu wa mali unaosababishwa na migogoro ya wakulima na wafugaji. Jumla ya matukio 42 ya migogoro yaliripotiwa kutoka Mikoa ifuatayo: Arusha (2), Dodoma (2), Geita (2), Kagera (2), Kigoma (2),  Manyara (2), Mbeya (3), Morogoro (8), Mtwara (1), Lindi (1), Pwani (8), Rukwa (1), Simiyu (2), Singida (1), Songwe (1), Tabora (1) na Tanga (3).

 

 1. Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti uvunjifu wa amani unaotokana na migogoro hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Vijiji, Kata, Wilaya na Mikoa limefanya mikutano katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya, Mara, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani na Shinyanga. Kupitia mikutano hiyo Jeshi la Polisi limetoa elimu kwa wananchi kuhusu njia mbalimbali za kuiepuka na kuikabili migogoro hiyo. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na kamati hizo pamoja na mamlaka nyingine ili kuzuia matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.

 
Mafunzo kwa Askari wa Jeshi la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuwaongezea ujuzi wa utendaji kazi jumla ya askari 956 wa Jeshi la Polisi wa vyeo mbalimbali walihudhuria mafunzo ya huduma bora kwa jamii, mbinu za upelelezi na mafunzo ya mbinu mbalimbali za kijeshi.  Kati ya hao, askari 137 walipata mafunzo nje ya nchi kwa ufadhili wa nchi za Marekani (55), India (5), China (25), Morocco (30), Misri (19), Uingereza (2), Japan (1) na askari 819 wamepata mafunzo ndani ya nchi zikiwemo kozi zilizofadhiliwa na nchi za Marekani, Canada, Korea Kusini, Ujerumani na Uturuki.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi lilifanya Kikao cha Kazi kuanzia tarehe 27 hadi 29 Machi, 2017 mjini Dodoma kwa lengo la kutathmini utendaji wake. Kikao hicho kilihusisha Maafisa Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi (Dar es Salaam na Zanzibar) na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi. Kauli Mbiu ya kikao hicho ilikuwa ni “Zingatia Maadili Tunapopambana na Uhalifu ili Kuimarisha Usalama kwa Maendeleo ya Taifa”Kupitia kikao hicho, Maazimio mbalimbali yalitolewa kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi nchi nzima.

 
Kuboresha Vitendea Kazi katika Jeshi la Polisi
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi, limeendelea kuimarisha na kuboresha zana za kazi za kisasa ambapo matengenezo makubwa ya Helkopta yamefanyika. Aidha, magari 77 kutoka Kampuni ya Ashok Leyland kwa ajili ya kazi mbalimbali za Jeshi la Polisi yamepatikana kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na India. Magari mengine 596 yanatarajiwa kuwasili mwaka 2017/18.

 
 
Usimamizi wa Nidhamu kwa Askari
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea kuwatambua maafisa, wakaguzi, askari na watumishi raia wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuwapa tuzo na zawadi. Jumla ya askari na watumishi raia 200 wamepewa tuzo kwa utendaji mzuri na kuliletea sifa Jeshi la Polisi katika nyanja mbalimbali. Aidha, fedha taslimu Shilingi 20,280,000 zilitolewa kwa watendaji 26, vyeti 119 na barua za pongezi 55 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mara, Tanga, Lindi, Geita, Katavi na Kikosi cha Ujenzi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kuwatambua na kuwatunuku zawadi Maafisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi raia watakaoendelea kufanya majukumu yao kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia nidhamu, Jeshi la Polisi limechukua hatua za kinidhamu kwa askari waliokiuka sheria za maadili ya kijeshi. Katika mwaka 2016/17 askari 14 na maofisa wawili (2) wamefukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali yakiwemo: rushwa, wizi, kubaka, utoro kazini, kughushi nyaraka na kujipa likizo.  Aidha, wakaguzi na maofisa 16 walipewa barua za kujieleza, sita (6) walipewa barua za onyo, kumi (10) walishtakiwa na wanne (4) walishushwa vyeo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi pia litaendelea kufanya uhakiki wa kina kwa ajira za askari wapya waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa na kuomba kujiunga na Jeshi la Polisi ili kuwa na askari wenye nidhamu na moyo wa dhati wa kulitumikia Taifa. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia nidhamu kwa askari wake ili kuongeza tija na ufanisi.

 
JESHI LA MAGEREZA
 
Programu za Urekebishaji wa Wafungwa
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Magereza limeendelea kutekeleza jukumu la kurekebisha wafungwa magerezani kwa kupitia program mbalimbali za mafunzo ya darasani, dini, michezo, ushauri nasaha na stadi za kazi. Stadi za kazi zilizotolewa ni pamoja na maeneo ya ujenzi, viwanda, kilimo, mifugo na utunzaji wa mazingira. Aidha, kupitia urekebishaji kwa stadi za kazi, ng’ombe wa nyama 8,381, ngombe wa maziwa 2,726, mbuzi 3,274, kondoo 503 pamoja na mifugo mingine iliendelea kuhudumiwa kwa kuboresha huduma mbalimbali za mifugo kama vile chanjo, dawa za tiba na huduma za kuogeshea mifugo kwenye Magereza yote yaliyo na mifugo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza litaendelea na program za kurekebisha wafungwa kwa kuhudumia jumla ya Ng’ombe wa nyama 9,958 na Ng’ombe wa maziwa 3,351, Mbuzi 3,898 na Kondoo 589 pamoja na wanyama wengine wadogo wadogo kwa kununua chanjo na tiba pamoja na kuboresha mashamba ya malisho.

 
 
 
Uimarishaji wa Viwanda vya Ndani
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeendelea na program za urekebishaji wafungwa kupitia viwanda vidogo vidogo kwa kuwapatia stadi za kazi kama vile: useremala katika Magereza ya Ukonga (Dar es Salaam), Uyui (Tabora) na Arusha (Arusha); utengenezaji wa sabuni katika Gereza la Ruanda (Mbeya); utengenezaji wa viatu katika Gereza la Karanga (Kilimanjaro); sanaa za mikono na uchongaji wa vinyago katika Gereza la Lilungu (Mtwara); ushonaji wa nguo katika Magereza ya Ukonga (Dar es Salaam) na Butimba (Mwanza); utengenezaji na uchakataji wa chumvi katika Gereza la Lindi (Lindi) na Lilungu (Mtwara).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza limeendelea kuimarisha Viwanda vidogo vidogo kwa kuingia ubia na Mifuko ya Hifadhi za Jamii ya National Social Security Fund (NSSF) na Parastatal Pensional Fund (PPF). NSSF imewekeza katika kilimo cha miwa na kufufua Kiwanda cha Sukari katika Gereza Mbigiri – Morogoro na PPF imewekeza katika Kiwanda cha Viatu, ambapo itafanya upanuzi wa kiwanda kwa kujenga kiwanda kipya cha kuchakata ngozi katika Gereza la Karanga – Kilimanjaro. Ubia huu utaboresha zaidi shughuli za uzalishaji mali zikiwemo bidhaa za sukari, viatu na ngozi na hivyo kutekeleza kwa vitendo jitihada za Serikali za kuelekea katika Uchumi wa Viwanda.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza linatarajia kuanzisha viwanda vipya katika Gereza Ukonga – Dar es Salaam kwa kutengeneza Kofia ngumu (Helmet) na kiwanda cha useremala katika Gereza la Isanga (Dodoma), ambapo jumla ya Shilingi 1,600,000,000 zimetengwa kwa ajili ya uanzishwaji wa viwanda hivyo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya ziara ya kutembelea viwanda vya nguo vya Namera Group of Industries (T) Limited (ambao ni muungano wa Namera Company Limited & Nida Garments Company Limited), 21st Century (Morogoro), Sunflag (Arusha) na Tanzania – China Friendship Textile Company Limited (URAFIKI – Dar es Salaam) ili kuona uwezekano wa kuzalisha sare za askari ndani ya nchi badala ya kuagiza sare hizo nje ya nchi. Baada ya ziara hiyo, viwanda hivyo viliwasilisha sampuli za vitambaa kwa Maboharia Wakuu wa Majeshi kwa ajili ya kuangaliwa ubora wake. Hatua hii ni miongoni mwa mkakati wa kukuza viwanda vya ndani.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Ofisi ya Boharia Mkuu wa Serikali imeridhika na ubora wa viatu vinavyozalishwa na baadhi ya viwanda nchini kwa matumizi ya askari. Viwanda hivyo ni Open Sanit kilichopo Tabata, Ital Shoes cha Kigamboni na Kiwanda cha Viatu cha Jeshi la Magereza kilichopo Gereza la Karanga Moshi.

 
Ukarabati wa Majengo na Miundombinu ya Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza linatarajia kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu ya Magereza pamoja na makazi ya askari yaliyoharibika na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera na mvua kali katika Magereza ya Kanegere (Geita), Bariadi (Simiyu), Mahabusu ya Morogoro na Mkono wa Mara (Morogoro), Manyoni (Singida), Lindi, Ubena na Kibiti (Pwani).

 
Upanuzi, Ukamilishaji, Ukarabati na Ujenzi wa Mabweni ya Wafungwa
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Magereza limeendelea na jitihada za kupunguza msongamano kwa kuanza ujenzi wa mabweni mawili (2) ya wafungwa katika Magereza ya Ruangwa – Lindi; kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu ya Magereza ya Kilosa, Mahabusu ya Morogoro, Mpwapwa, Lindi na Bagamoyo; kuanza ujenzi wa jengo la utawala pamoja na kukamilisha ujenzi wa bweni moja (1) katika Gereza la Chato – Geita. Aidha, ukarabati na uboreshaji wa majengo na miundombinu ya magereza yenye ulinzi mkali umefanyika sambamba na kukarabati mfumo wa maji taka katika Magereza ya Keko na Segerea. 

             
 
Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (Prison Corporation Sole) limeendelea na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo, mifugo na viwanda vidogo vidogo. Aidha, Shirika limepokea zabuni ya kutengeneza samani za ofisi za Waheshimiwa Wabunge zenye thamani ya Shilingi 2,807,127,174.50 ambapo mpaka sasa jumla ya Majimbo 18 yamepokea samani hizo. Pamoja na hilo, kazi ya utengenezaji wa madawati 30,000 imekamilika na yanaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza linatarajia kuongeza shughuli za uzalishaji kwa kuingia ubia na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kupata mtaji wa kutosha kuweza kukidhi soko la bidhaa zitokanazo na kilimo, mifugo, samani za ofisi na nyumbani, bidhaa za ngozi na shughuli za ujenzi.

 
 
 
Mafunzo katika Jeshi la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, mafunzo ya utawala, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za magereza na taaluma mbalimbali yanaendelea kutolewa kwa watumishi na askari 1,612 wa Jeshi la Magereza. Kati ya hao, askari watano (5) walipata mafunzo nchini Morocco kwa ufadhili wa Serikali ya nchi hiyo pamoja na askari na watumishi raia 880 wanaendelea na mafunzo katika vyuo mbalimbali ndani ya nchi katika vyuo vya Magereza.

 

 1. Mheshimiwa Spika, mafunzo hayo yatasaidia kuongeza weledi na kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika Jeshi la Magereza na pia kusimamia vema program za urekebishaji wa wafungwa magerezani. Katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza linatarajia kutoa mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa askari 1,530.

 
 
 
 
Upatikanaji wa Zana za Kisasa katika Jeshi la Magereza
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza limepanga: kununua mashine ishirini (20) za Kiwanda kipya cha Seremala katika Gereza la Isanga (Dodoma); ununuzi wa mashine tatu (3) kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya mawese na mise katika Kambi ya Kimbiji (Dar es Salaam); na mashine moja (1) ya uchakataji chumvi katika Gereza la Lindi (Machole).

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Magereza linategemea kupata mkopo wa matrekta 50 kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (National Development Corporation – NDC)  ambayo yatatumika katika kilimo kwenye mashamba ya Magereza ya Mollo (Rukwa); Songwe, Katai (Ruvuma); Kitengule (Kagera); Arusha; Kwitanga (Kigoma); Kambi Kimbiji (Dar es Salaam); Mugumu (Mara); Ubena (Pwani); na Idete, Kingolwira na Mbigiri (Morogoro). Upatikanaji wa zana hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa lengo la kuanza kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani.

 
      Utunzaji na Hifadhi ya Mazingira
 

 1. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Hifadhi ya Mazingira na Upandaji miti ambao unatekelezwa na Jeshi la Magereza kwa ufadhili wa Tanzania Forest Fund unaendelea ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2017 jumla ya miti 1,107,220 ilipandwa katika Magereza ya Mgagao na Isupilo – Iringa, Gereza la Mkwaya – Ruvuma, Gereza la Msalato - Dodoma, Gereza la Bariadi – Simiyu na Kambi ya Ihanga – Njombe.

 
PROGRAMU YA ADHABU MBADALA YA KIFUNGO CHA GEREZANI
 

 1. Mheshimiwa Spika, Programu ya Adhabu Mbadala ya Kifungo cha Gerezani hutekelezwa kupitia Makao Makuu ya Wizara. Program hiyo inahusisha upatikanaji wa Taarifa za Uchunguzi wa Kijamii. Katika kipindi cha mwezi Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya Taarifa za Uchunguzi wa Kijamii 2,376 ziliandaliwa na kuwezesha wafungwa 1,995 kunufaika na Programu ya Adhabu Mbadala ya Vifungo, ambapo wanaume ni 1,642 na wanawake ni 353. Miongoni mwa wafungwa hao, 456 wametumikia adhabu ya Probesheni na wafungwa 1,539 wametumikia adhabu ya Huduma kwa Jamii kwa kufanya kazi za kijamii kwenye Taasisi za Serikali. Hivyo, kupunguza gharama za uendeshaji katika magereza na taasisi husika. Aidha, wafungwa 794 wamemaliza adhabu zao na kurudishwa kwenye jamii kuungana na familia zao.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa sasa Idara ya Probesheni na Huduma kwa Jamii ina uwezo wa kuwatoa Gerezani/Mahakamani na kuwasimamia wafungwa 6,000 wenye sifa za kutumikia vifungo vya nje kwa mwaka. Kuendelea kuwepo kwa wafungwa 6,000 magerezani wenye sifa za kutumikia vifungo vya nje kunaigharimu Serikali takriban Shilingi 3,285,000,000 kwa mwaka ikiwa ni gharama za chakula za kuwahudumia wakiwa magerezani. Kiasi hicho cha fedha kingeweza kuokolewa endapo wafungwa hao wangetumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kutumikia adhabu mbadala katika Wizara na Taasisi za Umma.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo Serikali katika mwaka 2017/18 imetenga jumla ya Shilingi 1,045,586,000 ili kuongeza idadi ya wafungwa wanaotumikia vifungo nje ya magereza hadi kufikia takribani wafungwa 4,000.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa matumizi ya adhabu mbadala nchini, katika mwaka 2017/18 Wizara inatarajia kuongeza mikoa saba (7) iliyokuwa imebaki ambayo ni Kigoma, Rukwa, Katavi, Lindi, Ruvuma, Kagera na Simiyu. Hivyo, kufanya mikoa yote ya Tanzania Bara kutekeleza programu hiyo.

 
IDARA YA UHAMIAJI
 
Hali ya Ulinzi na Usalama Mipakani
 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa huduma kwenye mipaka kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini kwa mujibu wa Sheria za Uhamiaji. Katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya wageni 1,032,978 waliingia nchini ikilinganishwa na wageni 1,187,490 walioingia nchini katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016. Hadi kufikia Machi, 2017 jumla ya wageni 881,478 walitoka nchini ikilinganishwa na wageni 1,199,995 waliotoka nchini katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16.

 
Udhibiti wa Wahamiaji Haramu
 

 1. Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti wahamiaji haramu nchini, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, jumla ya watuhumiwa 9,581 wa uhamiaji haramu walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikilinganishwa na wahamiaji haramu 6,600 waliokamatwa katika kipindi Julai, 2015 hadi Machi, 2016. Hivyo, idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa imeongezeka kwa asilimia 45. Aidha, katika kipindi hicho Watanzania 5,923 walirudishwa nchini kati yao 253 ni stow aways na 5,670 ni Watanzania waliokuwa wakiishi nchini Msumbiji kinyume cha utaratibu.

Vibali Vilivyotolewa kwa Wageni Wakaazi
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, jumla ya wageni 11,259 wamepewa vibali vya ukaazi kwa mchanganuo ufuatao: Vibali Daraja “A” 2,474 ikilinganishwa na vibali 1,152 mwaka 2015/16 sawa na ongezeko la asilimia 114; Vibali Daraja “B” 6,736 ikilinganishwa na vibali 7,709 mwaka 2015/16 na Vibali Daraja “C” 2,049 ikilinganishwa na vibali 3,723 mwaka 2015/16.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vibali Daraja B na C vimepungua kutokana na zoezi la uhakiki wa uhalali wa utoaji wa vibali husika. Vibali hivyo vimetolewa kwa wageni wawekezaji, wageni waliopata ajira katika kampuni mbalimbali na walioingia nchini kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uhamiaji. Vilevile, hadi kufikia mwezi Machi, 2017 jumla ya Hati za Mfuasi 650 na Hati za Msamaha 1,427 zilitolewa.

 
 
Utolewaji wa Pasipoti na Hati nyingine za Safari
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017, jumla ya pasipoti 55,573 zilitolewa kwa Watanzania waliotaka kusafiri nje ya nchi kwa madhumuni mbalimbali ikilinganishwa na pasipoti 85,758 zilizotolewa katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016. Kati ya pasipoti zilizotolewa, pasipoti za kawaida ni 54,503 pasipoti za Afrika Mashariki ni 785, pasipoti za Kibalozi 229 na pasipoti za kiutumishi ni 56. Aidha, katika kipindi hicho Hati za Dharura za Safari 80,445 zilitolewa.  

 

 1. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji imeanza kutekeleza mfumo wa uhamiaji mtandao (e – immigration) kwa kufanya maboresho katika mtambo wa utoaji Pasipoti ili kuweza kutoa pasipoti za kielektroniki. Aidha, katika mwaka 2017/18 Idara ya Uhamiaji itaendelea kutekeleza mradi wa Uhamiaji Mtandao, kwa awamu kwa kuanza kutoa pasipoti za kielektroniki (e - passport).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango ipo katika hatua ya kukamilisha mfumo wa kulipia huduma mbalimbali za uhamiaji kwa njia ya ki-elektroniki. Mfumo huo utawawezesha wateja kulipia huduma hizo kwa njia ya simu sambamba na mifumo mingine iliyopo. Kwa sasa Idara ya Uhamiaji inafanya majaribio ya mfumo huo kwa kulipia baadhi ya huduma zake kama vile Hati za Ukaazi na Pasipoti. Aidha, mfumo huu utakapokamilika utaongeza udhibiti wa maduhuli ya Serikali.

 
Wageni Walioomba na Kupewa Uraia wa Tanzania
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 wageni 110 kutoka katika mataifa yafuatayo walipewa uraia: India (64), Yemeni (15), Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (5), Burundi (4), Kenya (5), Rwanda (5), Uingereza (3), Somalia (2), Congo (2), Ujerumani (1), Nigeria (1), Zambia (1), Poland (1) na Lebanon (1).

 
Watanzania Waliopatiwa Uraia wa Mataifa Mengine
 

 1. Mheshimiwa Spika, Watanzania 35 waliukana uraia wao baada ya kujipatia uraia wa mataifa mengine katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017. Mchanganuo wa Mataifa walikopata uraia ni kama ifuatavyo: Ujerumani (7), Uingereza (2), Norway (10), Sweden (3), Canada (1), Afrika Kusini (1), Zambia (1), Uganda (2), Marekani (1), Ureno (1), India (4), Botswana (1) na Srilanka (1). Kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357 Toleo la Mwaka 2002, watu hao wamepoteza hadhi ya kuwa raia wa Tanzania.

 
Mafunzo katika Idara ya Uhamiaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, jumla ya askari 35 wa Idara ya Uhamiaji walipata mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi. Kati ya hao, 10 walihudhuria mafunzo nchini Morocco na 25 nchini China kwa ufadhili wa Serikali za nchi hizo.

 
JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI
 
Ukaguzi wa Tahadhari na Kinga ya Moto
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016  hadi Machi, 2017 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea na zoezi la ukaguzi wa tahadhari na kinga ya moto nchini. Jumla ya maeneo 54,961 yalikaguliwa katika kipindi husika. Aidha, zoezi hili linaenda sambamba na utoaji elimu ya kujikinga na majanga ya moto na namna ya kutumia vifaa vya kuzimia moto.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaendelea na ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto na majanga katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha tahadhari na kinga dhidi ya moto na majanga mengine inazingatiwa.

 
 
Matukio ya Moto na Majanga Mengine
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshiriki kuzima moto na kufanya maokozi katika matukio 1,509 kwenye maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kutokana na kukithiri kwa matukio ya moto katika shule za bweni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kipindi hicho limefanya operesheni maalum na kufanikiwa kutoa mafunzo kwa shule za bweni 210 nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji litaongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za zimamoto na uokoaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo luninga, redio na magazeti. Aidha, elimu itaendela kutolewa kuhusu ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu zikiwemo shule, masoko, vituo vya mabasi, vivuko na taasisi mbalimbali.

 
Ununuzi wa Zana na Vifaa vya Kuzimia Moto
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepokea msaada wa vifaa mbalimbali vya kuzimia moto kutoka Ujerumani vyenye thamani ya Euro 45,000. Aidha, Wizara inakamilisha taratibu za ununuzi wa magari mawili (2) ya kuzimia moto.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Jeshi la Zimamoto litaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo ununuzi wa magari manne (4) ya kuzimia moto pamoja na vifaa vingine vya kuzimia moto na uokoaji, ambapo Shilingi 3,500,000,000 zimetengwa. Pia, Wizara imeanza majadiliano ya awali ya mikopo yenye masharti nafuu kutoka nchi za Ubelgiji (Euro milioni 19) na Austria (Euro milioni 5) kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kuzimia moto na vifaa vya maokozi.

 
 
 
Mafunzo katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
 

 1. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kuwapatia mafunzo ya ualimu wa uwanjani askari 18 na maafisa watatu (3) katika Chuo cha Maafisa - Magereza, Ukonga. Pia, jumla ya watumishi 10 wanahudhuria mafunzo ya kisasa ya kuzima moto na uokoaji nchini Morocco kwa ufadhili wa nchi hiyo, kati ya hao maafisa ni wanne (4) na askari ni sita (6).

 
MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
 
Kuendelea na Zoezi la Uandikishaji na Utoaji wa Vitambulisho vya Taifa
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Wizara kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeendelea kutekeleza lengo la Ibara 145 (f) ya Ilani ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 la kuendelea kuandikisha na kutoa Vitambulisho vya Taifa. Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 NIDA imesajili na kutambua jumla ya wananchi 8,551,259 na wageni 8,412 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza wigo wa kukamilisha zoezi hilo nchi nzima, Serikali imehamisha miundombinu ya taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwenda NIDA, ambapo uhakiki wa taarifa zilizochukuliwa unaendelea. Hatua hii itaongeza idadi ya wananchi waliosajiliwa nchini na kuruhusu matumizi mapana ya Vitambulisho vya Taifa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanikisha zoezi la kuwasajili na kuwahakiki watumishi wa umma 507,026 ambapo mfumo wa taarifa wa NIDA na ule wa taarifa za kiutumishi na mishahara Serikalini (Human Capital Management Information System – HCMIS) imeanza kubadilishana taarifa. Hatua hii itaiwezesha Serikali kulipa mishahara kwa watumishi sahihi na taarifa za watumishi kuendelea kuhuishwa kila mara. Aidha, Mfumo wa Vitambulisho vya Taifa umeanza kufanya kazi katika baadhi ya Benki nchini kama CRDB, Bank of Africa na Barclays.

 

 1. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, NIDA imenunua scanner 478 na imefunga mtandao wa mawasiliano katika wilaya 84 za mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mamlaka inaendelea na ufungaji wa mtandao wa mawasiliano katika wilaya 67 pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Kitambulisho cha Taifa.

 

 1. Mheshimiwa spika, katika mwaka 2017/18 NIDA itaendelea na zoezi la usajili na utambuzi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Watanzania milioni 22.7 wanatarajiwa kusajiliwa na kupewa Vitambulisho vya Taifa ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba, 2018. Aidha, Mamlaka itakamilisha ujenzi wa ofisi 13 za wilaya, itakamilisha uwekaji wa mtandao wa mawasiliano katika wilaya 135 ili kurahisisha utumaji wa taarifa za wananchi kutoka wilayani, itakamilisha kituo cha uchakataji, uzalishaji na utunzaji wa kumbukumbu (Data centre) na kituo cha uokozi wakati wa majanga (Disaster recovery centre).

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Mamlaka inatarajia kukarabati ofisi za usajili kwa baadhi ya wilaya na ununuzi wa vifaa vya kielektroniki kwa ajili ya kuunganisha mtandao wa mawasiliano. Aidha, Mamlaka itakamilisha utaratibu utakaoruhusu taasisi na mashirika mengi zaidi kutumia mfumo huu kupata taarifa sahihi za watu na kupunguza urasimu katika utoaji huduma.

 
  HUDUMA KWA WAKIMBIZI
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine, imeendelea kutoa hifadhi na huduma kwa wakimbizi kutoka nchi jirani, hususan zile za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la wakimbizi hao. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017 idadi ya wakimbizi nchini ilikuwa ni 340,835 na wamehifadhiwa katika kambi za Nyarugusu, Nduta, Mtendeli zilizoko Mkoani Kigoma, wengine katika makazi ya Katumba, Mishamo, Ulyankulu na Chogo (hawa ni wale waliokosa fursa ya kupata uraia wa Tanzania).

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kupokea wakimbizi wapya kutoka katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Awali, wakimbizi kutoka Burundi walikuwa wakipokelewa moja kwa moja kwenye kambi bila ya kufanyiwa mahojiano ya kina kutokana na kuingia kwa makundi makubwa kwa sababu ya machafuko ya kisiasa yaliyokuwa yanaendelea nchini kwao.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, imebainika kuwa hali ya usalama nchini Burundi imeimarika kwa sasa na wengi wa wakimbizi hawa wanakimbilia Tanzania kwa sababu za kiuchumi, hususan kutokana na ukame ulioikumba sehemu kubwa ya nchi hiyo na kusababisha njaa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, mwezi Februari, 2017 Serikali ilisitisha utaratibu wa kuwapokea na kuwasajili wakimbizi bila ya kuwahoji kwa kina (prima facie recognition) na kuendelea na utaratibu wa kawaida wa kila mkimbizi kuhojiwa na Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kujadili Maombi ya Waomba Hifadhi (National Eligibility Committee).  Lengo la utaratibu huu wa kumhoji kila muomba hifadhi ya ukimbizi ni kuhakikisha kuwa Serikali inatoa hifadhi ya ukimbizi kwa wanaostahili tu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali iliahidi kutekeleza miradi inayolenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia, fito za kujengea na kuhamasisha upandaji wa miti katika maeneo ya ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo. Katika kutekeleza azma hiyo, napenda kulifahamisha Bunge lako kuwa Wizara, kwa kushirikiana na UNHCR imeanza kutekeleza mradi wa kutumia majiko ya gesi kupikia badala ya kuni katika kambi ya Nyarugusu kwa awamu ya kwanza, ambapo mitungi ya gesi 3,216 imegawiwa kwa wakimbizi. Mradi huu utakuwa unafanyika kwa awamu hadi kufikia kambi zote za wakimbizi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi wa matumizi ya majiko ya gesi, miche ya miti 1,481,592 imekuzwa na kupandwa ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo. Aidha, ujenzi wa nyumba 15,664 ambazo zitatumia tofali mbichi na kuezekwa kwa mabati badala ya kutumia fito za miti ambazo zinachangia katika uharibifu wa mazingira unaendelea. Vilevile, majiko sanifu 59,924 yaligawiwa kwa kila nyumba katika kambi za Wakimbizi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara itaendelea kukabiliana na uharibifu wa mazingira katika maeneo ya kambi za wakimbizi. Pia, Wizara itaanza kutekeleza mradi wa matumizi mbadala ya mkaa katika kambi za wakimbizi, kufuatia kukamilika kwa utafiti wa upatikanaji wa malighafi za uzalishaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) inaendelea kutekeleza mradi wa kuwahamishia nchini Marekani wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wanaishi katika kambi ya Nyarungusu, ambapo kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, 2017 wakimbizi 6,545 walikuwa wamehamishiwa nchini humo.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na mpango wa kuwapeleka wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Marekani, wakimbizi 227 walihamishiwa katika nchi za Australia (23), Canada (197), Uingereza wawili (2) na Sweden watano (5).  Hata hivyo, sababu ya kuwahamishia wakimbizi nchi hizo ni kuzipunguzia mzigo nchi zenye wakimbizi wengi ikiwemo Tanzania.

 

 1. Mheshimwa Spika, kwa kuwa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo nchini Burundi imeimarika, Serikali imependekeza kuwepo kwa mazungumzo kati yake na Serikali ya Burundi pamoja na UNHCR. Lengo likiwa ni kuwawezesha wakimbizi watakaopenda kurejea kwao kwa hiari na kusaidiwa kujenga maisha mapya katika nchi yao ya asili.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 UNHCR kwa kushirikiana na NIDA imeanza zoezi la kuwasajili wakimbizi wanaoishi nchini. Katika hatua ya awali zoezi litahusisha kuwapatia namba za utambuzi ili kubana mianya ya wakimbizi kudanganya na kusajiliwa kama raia. NIDA imepanga kutekeleza zoezi hilo kabla ya kuanza usajili wa raia wa Tanzania katika Mkoa wa Kigoma ambako kuna kambi nyingi za wakimbizi. Lengo ni kuwapatia wakimbizi hao Vitambulisho vya Taifa vitakavyowawezesha kupata huduma mbalimbali wanazostahili.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kuwapatia wakimbizi hati za utambulisho pamoja na kusaidia utambulisho ni kutekeleza mikataba ya kimataifa ambapo wakimbizi wanapaswa wawe na hati muhimu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa uraia kwa wakimbizi 162,156 wenye asili ya Burundi walioingia nchini mwaka 1972 na kupangiwa kuishi katika makazi ya Katumba, Mishamo mkoani Katavi na Ulyankulu mkoani Tabora. Kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa utangamanisho (local integration), ambao utawahamasisha raia hao kuhamia katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Kutokana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kutimiza wajibu wake katika kutekeleza mradi wa utangamanisho kwa kuchangia rasilimali zinazohitajika kuwezesha raia hao kuwa sehemu ya jamii watakayohamishiwa.

 
VITA DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI WA   BINADAMU
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Sekretarieti ya Kupambana na Kudhibiti Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu iliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 17 wa makosa ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu na kuwafikisha mahakamani ili kuchukuliwa hatua za kisheria. Vilevile, wahanga 20 wa biashara hiyo waliokolewa, kusaidiwa na hatimaye kuunganishwa na familia zao.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Sekretarieti hiyo pia iliratibu mafunzo yaliyotolewa kwa maafisa 60 kutoka kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria, ambavyo ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa namna ya kupeleleza, kuendesha na kutoa maamuzi sahihi dhidi ya makosa ya biashara haramu ya binadamu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Sekretarieti imejipanga kuendelea kuratibu uendeshaji wa mafunzo kwa maofisa kutoka vyombo vinavyosimamia sheria na wadau wengine wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu. Sekretarieti pia itapitia sheria zinazotoa mwanya kwa wale wanaojihusisha na biashara haramu ya usafirishaji binadamu na kupendekeza kwa Serikali maeneo ya kufanyiwa marekebisho.

 
UTARATIBU WA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Wizara ilipokea malalamiko 392 kutoka kwa wananchi wakilalamikia utendaji wa vyombo vya kijeshi ndani ya Wizara. Aidha, Wizara ilifanya uchunguzi wa malalamiko hayo na jumla ya malalamiko 182 yalipatiwa ufumbuzi na wahusika kujulishwa na mengine 210 yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa. Katika mwaka 2017/18 Wizara itaendelea kushughulikia malalamiko ya wananchi na watumishi wa Wizara pamoja na kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini ukweli wa malalamiko hayo na kuchukua hatua stahiki.

 
 
USAJILI WA VYAMA VYA KIJAMII NA VYA KIDINI
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Wizara ilipokea jumla ya maombi 296 ya usajili wa vyama.  Kati ya maombi hayo jumla ya vyama 162 vimepewa usajili, maombi ya vyama 124 yanashughulikiwa na maombi ya vyama 10 yamekataliwa kutokana na kukosa sifa, kati ya hivyo vitano (5) ni vya kidini na vitano (5) ni vya kijamii.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sanjari na shughuli za usajili, Wizara imeanza kuchukua hatua za kuvifutia usajili vyama visivyotekeleza wajibu wao kulingana na sheria, ambapo vyama 13 vimepewa taarifa ya kusudio la kuvifuta. Katika mwaka 2017/18 Wizara itaendelea na usajili na uhakiki wa vyama vya kidini na kijamii ili kuwa na kanzi data yenye taarifa sahihi za vyama kwa lengo la uanzishwaji wake.

 
 
 
SHERIA, KANUNI, MIKAKATI INAYOHUSU WIZARA
 

 1. Mheshimwa Spika, katika mwaka 2016/17 Wizara imekamilisha uandaaji wa Mpango Mkakati kwa kipindi cha 2016/17 - 2020/21 ambao ni msingi wa utekelezaji wa malengo ya Wizara na uandaaji wa mpango na bajeti kwa kila mwaka wa fedha. Aidha, Rasimu ya Mpango wa Kudhibiti Vihatarishi (Risk Register) kwa mwaka 2016/17 – 2020/21 imeandaliwa kwa lengo la kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa maeneo hatarishi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, Wizara imekamilisha Rasimu za Mapendekezo ya Kutunga Sheria Mpya ya Jeshi la Polisi Tanzania (The Tanzania Police Force Act, 2017) na Mapendekezo ya Kutunga Sheria Mpya ya Usajili na Utambuzi wa Watu (The Registration and Identification of Persons Act, 2017). Katika mwaka 2017/18 Wizara itaendelea kuboresha sera, sheria, kanuni na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.

 
MAENDELEO YA RASILIMALI WATU NA AJIRA MPYA
 
Mafunzo kwa Watumishi wa Wizara
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwaongezea ujuzi watumishi waliopo Makao Makuu ya Wizara kwa kuwawezesha kupata mafunzo ndani ya nchi. Katika mwaka 2016/17 watumishi kumi (10) walipatiwa mafunzo ndani ya nchi katika fani za makarani masijala, katibu muhtasi pamoja na fani ya usafirishaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara inatarajia kuwapeleka mafunzoni ndani ya nchi jumla ya watumishi 141 wa kada mbalimbali waliopo Makao Makuu ya Wizara. Kati ya hao, watumishi 120 watahudhuria mafunzo ya muda mfupi na watumishi 21 mafunzo ya muda mrefu.

 
 
 
 
Ajira Mpya kwa Mwaka 2017/18 na Upandishwaji Vyeo
 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla wake inatarajia kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 7,317. Kati ya hao watumishi 105 ni wa Makao Makuu ya Wizara; askari 5,772 wa Jeshi la Polisi; na askari 1,440 wa Idara ya Uhamiaji.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 4,339 (Makao Makuu ya Wizara 26, Jeshi la Polisi 2,573, Jeshi la Magereza 500, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 600, Idara ya Uhamiaji 600 na NIDA 40). Aidha, Wizara itaendelea kuwapandisha vyeo watumishi na askari kadiri watakavyopata sifa kulingana na miundo yao ya kiutumishi.

 
MAPAMBANO DHIDI YA MAAMBUKIZI YA VVU/UKIMWI
 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Wizara imeendelea na juhudi mbalimbali za kupambana na  janga la UKIMWI  zikiwemo za kuboresha huduma za upimaji wa Virusi vya UKIMWI (VVU) na ushauri nasaha ili  kuhakikisha huduma  hizo zinawafikia watumishi, askari, wafungwa na familia za askari na zinapatikana bure pamoja na kampeni za upimaji wa hiari wa mara kwa mara. Aidha, fedha za kila mwezi kwa askari na watumishi raia wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa ajili ya kuimarisha afya zao dhidi ya magonjwa nyemelezi ziliendelea kutolewa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Wizara kwa kushirikiana na Asasi ya John Snow Inc (JSI – Aids Free) ilitoa mafunzo kwa watumishi 55 ambao watakuwa waelimishaji wa masuala ya UKIMWI katika magereza nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18 Wizara itaendelea kutoa huduma kwa watumishi waathirika wa VVU na UKIMWI kulingana na miongozo ya Serikali. Aidha, watumishi wataendelea kuhamasishwa kupima afya zao mara kwa mara ili kuweza kupata matibabu na ushauri nasaha pale watakapogundulika kuwa na VVU/UKIMWI pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

 
SHUKRANI
 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni kwa kunipa ushirikiano katika kuongoza Wizara hii. Kipekee nawashukuru Katibu Mkuu Meja Jenerali Projest A. Rwegasira na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Hassan S. Yahya kwa kusimamia vema utekelezaji wa majukumu na utendaji kazi wa Wizara hii nyeti inayohusu usalama wa nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wakuu wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara nikianza na Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Bw. Ernest J. Mangu; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dkt. Juma A. Malewa; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bw. Thobias E. Andengenye; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna P. Makakala; na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Bw. Andrew W. Massawe. Pia, nawashukuru Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Bw. Abdulrahmani O. Kaniki, Makamishna; Makamishna Wasaidizi; Wakuu wa Idara, Vitengo na Sehemu; askari na wafanyakazi wote kwa utendaji wao uliowezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninatoa shukrani zangu kwa nchi wahisani ikiwemo Serikali za Nchi za China, India, Korea ya Kusini, Marekani, Misri, Ujerumani, Morocco, Uturuki na Taasisi na Mashirika mbalimbali ya ACSA, ADRA, AIRD, AU, CCBRT, CDF, CEMDO, Danish Refugee Council, DFID, EAC, EAPCCO, EU, GTI, Hanns Seidel Foundation, Help Age International, INTERPOL, IOM, IRC, John Snow Inc (JSI – Aids Free) OXFAM, Pharm Access, Plan International, REDESO, SADC, SARPCCO, Save the Children International, TRCS, TWESA, UNDP, UNFPA, UN – WOMEN, UNHCR, UNICEF, WFP, WLAC, TAWLA, TAYOA, TACAIDS, World Vision Tanzania, Taasisi za dini, vyombo vya habari, wananchi pamoja na wadau wengine kwa kutoa taarifa na misaada mbalimbali ambayo imesaidia katika utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa naishukuru familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi, hususan wa Jimbo langu la Iramba Magharibi kwa imani yao kwangu na ushirikiano wao katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya jimbo letu.

 

 1. HITIMISHO

 

 1. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuweka mipango bora ya kudhibiti matukio ya uhalifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola nchini na vya kimataifa pamoja na kuwashirikisha wananchi ili kuhakikisha uhalifu unadhibitiwa na hali ya usalama inaimarika nchini.

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 930,396,817,000 kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2017/18. Kati ya fedha hizo, Shilingi 890,388,452,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, ambapo Shilingi 367,706,884,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 522,681,568,000 ni Mishahara. Shilingi 40,008,365,000 ni fedha za Miradi ya Maendeleo, kati ya fedha hizo Shilingi 39,700,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 308,365,000 ni fedha za nje.

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 
 
Majedwali Mbalimbali
 

Back to Top