generica viagra

HOTUBA YA MHE. MWIGULU NCHEMBA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KATIKA KUFUNGUA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI CHA KUJADILI BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA 2017/2018

Friday, May 5, 2017

HOTUBA YA MHE. MWIGULU NCHEMBA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KATIKA KUFUNGUA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI CHA  KUJADILI BAJETI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA MWAKA 2017/2018

  • Balozi Hassan Simba Yahya, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
  • Makamishna Jenerali,
  • Makamishna,
  • Wakurugenzi wa Idara na Vitengo,
  • Katibu wa Baraza,
  • Viongozi wa TUGHE Taifa na Mkoa,
  • Wawakilishi wa Wafanyakazi,
  • Wawakilishi kutoka matawi yote ya TUGHE,
  • Wageni waalikwa,
  • Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kwa kutukutanisha hapa kwa mara ya kwanza tangu niteuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Hii inanipa sababu ya kuwashukuru sana waandaaji wa Kikao hiki na washiriki wote kwa ushiriki wenu, katika kikao hiki cha siku moja. Baraza hili ni hitajio muhimu la kisheria kwa utaratibu tuliojiwekea wa kuwashirikisha wafanyakazi katika kupanga mapato na matumizi na mipango ya maendeleo ya sekta hii ambayo Taifa limetupa jukumu la kusimamia.
Ndugu wajumbe,
Nitumie fursa hii pia, kuwashukuru watumishi wote wa Wizara yangu kwa namna mnavyonipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yangu.
Pamoja na changamoto za kibajeti tunazokabiliana nazo, mmendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika kuihudumia jamii, hili ni jambo la Kizalendo na linanipa kujivunia na kunipa Imani kufanya kazi katika Wizara hii ambayo ina jukumu la msingi la kulinda Usalama wa Raia na mali zao.
Ndugu wajumbe,
Kwa kuwa kikao hiki, kina ajenda maalum ya kujadili utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2016/2017 na Malengo ya mwaka 2017/2018 ni vema wajumbe mkatumia fursa hii vizuri ili matokeo ya majadiliano yenu yalete tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu. Baraza hili linatoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki moja kwa moja katika kupanga bajeti yao na hatimaye kuitekeleza.
Kikao hiki kinawapa fursa wajumbe wote kushiriki kikamilifu kwa kutoa michango yenu ya mawazo hivyo ninaamini mtatumia fursa hii vizuri, kwa ajili ya kukamilisha jukumu lenu hili muhimu na la kipekee. Sio nchi nyingi duniani zenye utaratibu huu mzuri wan chi yetu.
Kama alivyoagiza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi pale Moshi, hii ni fursa rasmi ya Wafanyakazi kupitia uwakilishi wenu, kuijadili na kuitolea maoni Bajeti ya Wizara tuliyopewa jukumu la kuisimamia.
Ndugu wajumbe,
Natoa wito kwa watumishi wote kushirikiana na kujituma kufanya kazi kwa bidii kila mtu kwa nafasi yake ili hatimaye Wizara yetu iweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa mwaka ujao wa fedha kwa maana kwa pamoja tunaweza.
Kwa maneno hayo machache natamka kwamba Kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha kujadili Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kimefunguliwa rasmi.
Nawatakia kila la kheri,
 
Asanteni kwa kunisikiliza.
 
 

Back to Top