WIKI YA KUMBUKIZI YA HAYATI MWALIMU NYERERE YAZINDULIWA RASMI
Ikiwa kila
Aprili 13 ni siku ya kuzaliwa kwa aliyekuwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere Taasisi ya Mwalimu Nyerere leo imezindua wiki ya kumbukizi ya
Hayati Mwalimu Nyerere ili kuhuisha falsafa ya maisha yake na kuhakikisha maisha
aliyoyaishi yanaendelezwa na kuenziwa kwa manufaa ya ustawi wa jamii na Nchi,
uzinduzi uliofanyika Mwitongo Wilayani Butiama.
Akifungua
wiki ya kumbukizi hiyo Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo
la Butiama ambapo ndipo alipozaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mhe. Jumanne Sagini
amesema kuwa falsafa za Mwalimu Nyerere kwetu sisi Watanzania zilienzi katika
kutetea Uhuru, Umoja, Kujitegemea, Haki, Utu, Heshima kwa binadamu, Usawa na
Demokrasia kwa kuwa muumini asiyetetereka katika misingi hiyo kwa hapa nchini
lakini pia katika siasa za dunia jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa
katika taswira ya Nchi ya Tanzania tunayoiona sasa.
“Msingi wa
fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere ulijengeka hapa Butiama. Jambo linaloleta
faraja ni kwamba fikra na maono mbalimbali ya Babab wa Taifa yametambuliwa na
kutekelezwa na awamu zote za Uongozi wa Nchi yetu. Maono ya Msingi ikiwemo
Umoja wa Taifa, Maendeleo ya Taifa,dhana ya kujitegemea,dhana ya kujituma
kufanya kazi vilikuwa ni vitu ambavyo vimethaminiwa na kuendelezwa ikiwa ni
sambamba na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati na kuhakikisha Mtanzania
anakombolewa kielimu na kiuchumi.”alisema Sagini
Katika hatua
nyingine Naibu Waziri Sagini amewataka Wazazi kuendelea kusimamia na kutekeleza
wajibu wa malezi ya Watoto ili kuendelea kusimamia maadili ya Taifa na kwa
kuzingatia Mila, Desturi na Tamaduni tulizorithishwa na Waasisi wa Taifa akiwemo
Hayati Mwalimu Nyerere.
Awali
akizungumza katika Uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere Profesa Francis Matambalya amesema kuwa licha ya kuwa na siku ya
kumbukizi ya Kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere ambayo huadhimishwa ifikapo 14
Oktoba ya kila mwaka siku hiyo imekuwa na shughuli nyingi za Kitaifa ikiwemo
kuzima mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na hivyo kuamua kuja na wiki ya
kumbukizi ili kuweza kutoa elimu zaidi kwa jamii na kurithisha mazuri yale yote
aliyoyafanya.
Kwa upande
wake Joseph Butiku ambaye ni miongoni mwa Waasisi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere
amesema kuwa mawazo aliyoyatumia Hayati Mwalimu Nyerere katika kujenga misingi
ya Taifa la Tanzania na kuweka sera za Nchi hii na kuwa na msimamo wa kupigania
haki kokote duniani ni mambo ambayo aliyaelekeza Hayati kuwa yapo Butiama na
ndio maana Taasisi hiyo imeamua kufika Butiama na kufanya majadiliano kuenzi
msimamo huo.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya
walioshiriki katika Uzinduzi huo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka,Mkuu
wa Wilaya ya Butiama Mwalimu Moses Kaegele
wamesema kuwa falsafa za Hayati Mwalimu Nyerere mpaka sasa zinaendlea
kuishi kwani kwa sasa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwaamini Vijana
katika nafasi mbalimblai za uongozi na pia kuendelea kuimarisha Amani na
utulivu wa Taifa