MASAUNI AZITAKA JUMUIYA ZA KIRAIA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI, AZINDUA KAMPENI ZA USAJILI NCHINI
SERIKALI imezitaka jumuiya za kiraia kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za maadili, uwazi, na uwajibikaji kuhakikisha wanachangia katika maendeleo ya jamii bila kuhatarisha ulinzi na usalama wa nchi au kusababisha mmonyoko wa maadili.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni katika ufunguzi wa kampeni za usajili wa jumuiya za nchini iliyobebwa na kauli mbiu isemayo 'Usajili wa Jumuiya kwa maemndeleo na ustawi wa taifa letu'.
"Katika kipindi cha karibuni kumeibuka wimbi la kutumia Jumuiya za Kiraia katika kufanya vitendo vinavyo hatarisha amani na Usalama wa Nchi yetu ambapo kuna baadhi ya Jumuiya zinatumika katika kusaidia makundi yenye dhima ya kigaidi, kusambaza propaganda za uchochezi, kuwasilisha agenda za kigeni au wafadhili wa nje ambazo zinaweza kuhatarisha maslahi ya Taifa ikiwemo mmonyoko wa maadili," alisema.
Masauni alisema serikali ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za Jumuiya za kiraia ikuhakikisha kuwa zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
"Pia kumebainika changamoto ya uanzishwaji holela na utitiri wa nyumba za ibada katika maeneo mbalimbali nchimi na baadhi ya Jumuiya za dini hususan makanisa na misikiti imebainika kujengwa katikati ya makazi ya watu, kuna mrundikano wa taasisi nyingi kwenye eneo dogo na baadhi ya taasisi kutumia sauti za juu na hivyo kusababisha adha na usumbufu katika jamii," alisema.
Vilevile, alisema baadhi ya Jumuiya za Kiraia zimeripotiwa kujihusisha au kutumika katika kufanikisha kutendeka kwa makosa ya jinai na vitendo vingine vyenye madhara kwa jamii.
Miongoni mwa makosa hayo ni utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa shughuli za kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha na uwepo wa Jumuiya za Kidini zinazotoa mafundisho potofu na hatarishi kwa usalama wa raia.
Alisema changamoto za aina hiyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika ushughulikiwaji wake ili kuendelea kudumisha hali ya utulivu na usalama katika maeneo yote nchini.
Hivyo aliwataka viongozi waliopewa dhamana ya kuwezesha ustawi wa jamii katika Mikoa yao ni kutambua kuwa wanao wajibu mkubwa wa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuondoa changamoto hizo katika jamii.
"Madhara yatokanayo na kuchelewa kutoa ufumbuzi wa changamoto nilizozitaja hapo juu pamoja na udhaifu wa mifumo ya Fedha katika taasisi hizo, umepelekea Taasisi ya Kimataifa ya Financial Action Task Force (FATF) ambayo ilianzishwa na Baraza ka usalama la umoja wa mataifa, kutoa ripoti ambayo inaonesha kuwa Nchi yetu haina mifumo mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji wa mienendo wa jumuiya za kiraia zikiwemo taasisi na madhehebu ya dini,"alisema.
Alisema kutengeneza mazingira rafiki ya taasisi hizo kutumika au kuwa katika hatari ya kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu au kufadhili masuala ya ugaidi na hali hiyo imesababisha Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu hivyo lazimaa kushirikiana kuondoa changamoto hizo.
"Kutokana na Taifa letu kuwekwa kwenye kundi hilo, vyombo vya Kimataifa na Wadau mbalimbali wa Kimataifa wamekuwa wakipewa tahadhari kuhusu udhaifu wa kusimamia Jumuiya hizi ambao unaweza kutumika katika masuala utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.
"Hali hii inaweza kuleta madhara ya kuharibu taswira nzuri ya kidiplomasia iliyopo katika nchi yetu, hivyo, naendelea kusisitiza umuhimu wenu wa katika kushirikiana kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya inatekeleza Mpango Kazi wa FATF utakaowezesha Serikali kuondolewa kwenye kundi hili na kufanikisha jukumu la kudumisha amani na utulivu katika maeneo yetu," alisema.
Pia alisema wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa karibu na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na Ofisi za Wakuu wa Wilaya katika ufuatiliaji wa mienendo na usimamizi wa jumuiya kupitia Kamati za Usalama zilizopo katika ngazi za mikoa na Wilaya.
Katika kutekeleza jukumu hilo, yafuatayo yamefanyika ikiwa uwasilishaji wa Taarifa juu ya mienendo hatarishi au migogoro ya jumuiya zilizopo katika maeneo husika na hatua zilizochukuliwa na Mamlaka za Serikali katika ngazi za Wilaya au Mikoa na kuendesha mazoezi ya Ukaguzi kwa kupita kamati za Usalama za Mikoa au Wilaya;
Pia kuwasilisha maoni na mapendekezo juu ya namna bora ya kuongeza ufanisi kwenye usajili na usimamizi wa jumuiya kulingana na mazingira na changamoto za kipekee zilizopo katika maeneo makundi ya kigaidi yanayoweza kuhusika kutumia jumuiya za kiraia kama njia ya kukusanya fedha kwa kisingizio cha kusaidia misaada au miradi ya maendeleo.
MSAJILI WA JUMUIYA ZA KIRAIA
Kwa upande wake Msajili wa Jumuia za Kiraia Nchini,Emmanuel Kihampa alisema hadi kufikia Januari mwaka huu kuna jumla taasisi za kiraia 10,690.
Wizara ya mambo ya ndani kupitia ofisi ya Msajili wa Jumuiya imekuwa iliendelea na uhakiki na uhishaji wa vyeti lengo likiwa kutambua jumuiya ambazo zipo hai na nyingine ambazo hazipo tena.