Tanzania logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

SAGINI AFUNGUA SEMINA YA SIKU TANO KUJADILI MPANGO WA USALAMA BARABARANI



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amefungua semina ya Siku Tano yenye lengo ya kubadilishana uzoefu wa namna ya kudhibiti ajali na kuwa na usalama barabarani ili kuondokana na madhira yanayoikumba jamii ikiwemo vifo na ulemavu.

Akizungumza wakati akifungua semina ya siku tano Novemba 27 hadi Disemba 2, mwaka huu ya Kanda ya Afrika kuhusu mpango wa usalama barabarani iliokutanisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Afrika Kusini, Burundi, Rwanda na Botswana iliondaliwa na Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utoaji wa elimu ya usalama barabarani la Tanzania Safety Roads Initiatives (TARSI) ameeleza kuwa ajali nchini zimepungua.

"Ajali za barabarani zimepungua ila sio kama awali na tunaendelea kudhibiti kwani mara nyingi zinatokana na sababu za kibinadamu kama dereva mwenyewe pia kuna matatizo ya vyombo vya moto vyenyewe, uchakavu na ubovu pamoja na miundombinu kuwa mibovu," amesema.

Mhe Sagini alifurahishwa na waandaji wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya vijana wa kitanzania na kuwaomba Watanzania kujifunza kutoka mataifa mengine ili watumie mafunzo hayo katika utekelezaji wa shughuli za kila siku kwenye matumizi ya barabara na vyombo vya moto.

Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini SACP Ramadhan Ng'anzi, ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za ukanda wa Afrika Mashariki zinazotajwa kupunguza ajali za barabarani baada ya kuweka mifumo madhubuti ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

"Tunaendelea vizuri na tangu Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aruhusu mabasi kusafiri usiku sasa hivi ni mwezi wa pili hatujasikia basi limepata ajali, mbali na ajali mbili kubwa zilizotokea hivi karibuni na zote zimetokea mchana, tunajitahidi kuangalia kwanini ajali zimetokea mchana lakini usiku hazijatokea hivyo imekuaje usiku wameweza tunajitahidi sana ili tufikie lengo la Tanzania bila ajali inawezekana," Ameeleza Ng'anzi.